Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI KALEMANI ASISITIZA TAASISI ZA UMMA VIJIJINI ZIWEKEWE UMEME

Na Veronica Simba – Dodoma

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani amewaagiza wataalamu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kuwasimamia wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini nchi nzima, kuhakikisha wanatoa kipaumbele cha kuunganisha umeme kwa taasisi zote za umma zilizo katika maeneo yao.

Alitoa maagizo hayo kwa nyakati tofauti wiki iliyopita akiwa katika ziara ya kazi wilayani Chamwino, Mkoa wa Dodoma, ambapo aliviwashia umeme vijiji vya Buigiri na Mwigamwile.

Akizungumza na wanafunzi wa shule ya sekondari Buigiri pamoja na wananchi, Waziri alisisitiza kwamba, kitendo cha kuwasha umeme katika shule hiyo kinalenga kutoa hamasa katika utekelezaji wa maagizo ya serikali kuwa taasisi zote za umma ni lazima zipelekewe umeme.

“Niwaombe viongozi wa Halmashauri za Vijiji na Wilaya nchini kote, kuhakikisha taasisi za umma katika maeneo yenu zinalipia gharama ya kuunganishiwa umeme ambayo ni shilingi 27,000 tu kwa ninyi mlioko vijijini, ili taasisi hizo zote ziunganishiwe umeme,” alisisitiza.

Aidha, kuhusu suala hilo la kulipia gharama za kuunganishiwa umeme, Waziri alilazimika kutoa msisitizo kwa viongozi na wananchi kwani alisema kumekuwepo na tabia ya baadhi ya watu kulalamika kuwa hawajaunganishiwa umeme lakini baada ya kufuatilia sababu iliyobainika ni kuwa wanakuwa hawajalipia huduma hiyo.

“Lipieni umeme. Msibaki kulalamika tu. Mlalamike mkiwa mmelipia.”

Katika hatua nyingine, Waziri Kalemani aliwataka wanafunzi wa Shule hiyo ya Buigiri kuongeza jitihada katika masomo kwani tayari wamepelekewa umeme ili kuongeza kiwango cha ufaulu shuleni hapo.

Awali, akizungumza wakati wa tukio hilo la uwashaji umeme, Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Vumilia Nyamoga alimweleza Waziri kuwa, Shule husika imekuwa na kiwango duni cha ufaulu kutokana na sababu mbalimbali, mojawapo ikiwa ni ukosefu wa umeme tangu ilipoanzishwa mwaka 2007.

Akiwa katika kijiji cha Mwigamwile, Waziri Kalemani aliwasha umeme katika Ofisi mpya ya Serikali ya Kijiji, ili kuendelea kutoa msisitizo wa azma ya serikali kuhakikisha taasisi za umma zinaunganishiwa umeme.

Aidha, ili kuonesha msisitizo zaidi, Waziri Kalemani, alilazimika kulipa yeyé mwenyewe shilingi 27,000 ikiwa ni gharama za kuunganisha umeme katika kisima cha maji kilichoko kijijini Ikoa, Kata ya Ikoa ambacho pamoja na kuwa kimekamilika kwa muda mrefu hakijaanza kufanya kazi kutokana na kutokuwa na umeme.

Waziri aliwaagiza wataalamu wa TANESCO kuunganishia kisima hicho umeme kabla ya Jumanne  Aprili 23 mwaka huu.

Katika maeneo yote ya Wilaya hiyo ambayo Waziri alipita kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, alimsisitiza Mkandarasi kuongeza kasi ya kuunganisha umeme ambapo alimtaka kufikia Desemba mwaka huu, awe amekamilisha kazi ya kuviunganishia umeme vijiji na vitongoji vyote vya Jimbo la Chilonwa.

Mbunge wa Jimbo hilo, ambaye alifuatana na Waziri katika ziara hiyo, Joel Mwaka, alimwambia kuwa vijiji 20 vya jimbo hilo kati ya 47 vilivyopo, havijafikiwa na umeme.

“Pamoja na kuwa mkataba unaonesha kazi hii ya kuunganisha umeme kupitia mradi wa Umeme Vijijini, Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Kwanza (REA III, Phase I) inatakiwa ifikie tamati Juni mwakani, lakini nakuagiza wewe mkandarasi ukamilishe kazi hii ifikapo Desemba,” alisisitiza Waziri.

Mbali na kuwasha umeme katika vijiji vya Buigiri na Mwegamile, Waziri pia alikagua utekelezaji wa miradi ya umeme katika vijiji vya Ikoa (Kata ya Ikoa), Nguga (Kata ya Msamalo) na Mlebe (Kata ya Msamalo).

Viongozi wengine walioshiriki ziara hiyo ni pamoja na Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Mbadala, Mhandisi Innocent Luoga, Kaimu Meneja wa TANESCO, Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Tumaini Nyari, pamoja na wahandisi wasimamizi wa miradi ya umeme vijijini kutoka wizarani na REA.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com