WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Jacob Kingu kumsimamisha kazi Mkuu wa Upelelezi wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Mbogwe (OC CID) Mkoani Geita, pamoja na Mkaguzi wa Jeshi hilo kwa kosa la kutuhumiwa kuomba na kupokea rushwa.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Kata za Ilolangulu na Busabaga wilayani humo, Lugola alisema Polisi hao ambao waliomba na kupokea rushwa ya shilingi milioni nne kutoka kwa wananchi wa Kata hizo ambao walikuwa wanataka kuwaombea dhamana ndugu zao, ndipo polisi hao wakaomba fedha kiasi hicho ili watolewe mahabusu ya Polisi katika Kituo cha Polisi Mbogwe.
Maafisa hao wa Polisi ambao wanadaiwa kupokea rushwa kutoka kwa wananchi hao ni OC CID wa Wilaya hiyo, Luitiko Kibanda na Mkaguzi wa Polisi aitwaye kwa jina la Kessy ambao wananchi hao pamoja na Mbunge wao walisema waliwakabidhi fedha kiasi hicho.
”Wananchi walipitisha mchango kila kaya ili kuwanusuru wenzao na viongozi wao haikutosha wakamuomba Mbunge wao akawachangia shilingi laki tano pia wakachukua na hela yao iliyokuwa ni ya kujengea zahanati wakawapelekea polisi, bila hata aibu polisi hawa wakachukua fedha hizo, bila kujali hali za kiuchumi walizonazo wananchi hao”alisema Lugola.
Lugola alisema licha ya Kata hizo kukithiri vitendo vya wizi na ubakaji na Polisi kufanya wajibu wao kuwakamata watuhumiwa mbalimbali, lakini ni kosa kuwaonea wananchi kwa kuwaomba rushwa kupitia kisingizio cha utoaji wa dhamana huku sheria ikieleza kwa makosa yanayodhaminika dhamana itolewe kwa mujibu wa sheria na siyo kuwanyanyasa wananchi.
Aidha, Waziri Lugola alitoa onyo kwa Polisi nchini ambao wanawafanya wananchi mtaji kwa kuwabambikiza kesi kisha kuwaomba pesa, kuacha tabia hiyo mara moja na endapo wakibainika hatawavumilia, hatawaonea huruma
hivyo sheria itafuata mkondo wake.
Kwa Upande wake Diwani wa Kata ya Ikobe, Wilayani humo, Costantine Kwezi, alimuomba Waziri kuwasaidia kukamilisha kituo cha polisi katika Kata yake na pia kuongeza idadi ya askari kituoni hapo, kwasababu kituo hicho kina askari mmoja ambaye anazidiwa na majukumu.
Baadhi ya kina mama katika mkutano huo, nao walimuomba Waziri huyo kuwasaidia waume zao waliokamatwa kwa kosa la kusingiziwa kuwa ni majambazi kuachiwa huru, kutokana na kukosa hela ya kuhudumia familia na wao wameachwa bila kazi na watoto wadogo.
Social Plugin