Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MKUU ASISITIZA WANAUME WAPIME VVU ILI WAJUE HADHI ZAO, WASITEGEMEE WAKE ZAO


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa Dodoma wajitokeze kwa wingi kuchangia damu ili iweze kutumika kuokoa maisha ya wengine.


Ametoa kauli hiyo hilo leo (Jumanne, Aprili 30, 2019) wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa Dodoma waliohudhuria kilele cha maadhimisho ya miaka 10 ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) yaliyofanyika kwenye viwanja vya Mwl. Nyerere, jijini Dodoma.

Amesema Serikali inaendelea na kampeni ya kuhakikisha vituo vya afya na hospitali vinakuwa na akiba ya kutosha ya damu kwa ajili ya wagonjwa wenye kuhitaji damu.

“Tunawasihi Watanzania waende kuchangia damu ili benki ya damu iwe na akiba ya kutosha endapo mtu ataenda pale kufanyiwa upasuaji na akapoteza damu nyingi, au awe amepata ajali au ameenda kujifungua, apate damu kwa haraka kutoka kwenye benki yetu,” amesisitiza.

Akitumia wingi wa watu kwenye hafla hiyo, Waziri Mkuu amesema: “Leo hii hapa Dodoma kuna hospitali kubwa ya Benjamin Mkapa kule UDOM, tuna vituo vya afya kama kile cha Makole vyote vinahitaji kutoa huduma hii lakini haitoshi. Tuliagiza kila penye mkusanyiko wa watu wengi, lazima kujengwe banda la kupima afya na kuchangia damu.”

Akizungumziai kuhusu upimaji wa virusi vya UKIMWI (VVU), Waziri Mkuu amesema kampeni inafanyika lakini kasoro iliyopo ni kwamba wanaojitokeza kwa wingi kupima afya zao ni wanawake na wanaume hawapimi. “Takwimu zilizopo zinaonyesha hivyo,” amesema.

“Mimi ndiye balozi wenu akinababa kwenye kampebi ya kitaita ya upimaji VVU. Nataka niwahimize twende leo tukapime, tusitegemee matokeo ya vipimo vya mke. Wengi mnasubiri matokeo ya mke, akisharudi kutoka kupima na kusema niko safi, basi na wewe unaanza kufurahi unasema niko safi, hapana!”

“Wanaume msijidanganye, nenda ukapime wewe mwenyewe ujijue afya yako na mkeo naye apime ajijue ili nyumba nzima iwe na uhakika kwamba mko salama. Kwa hiyo wanaume tukitoka hapa, twende tukapime,” alisema.

Mapema, Mkuu wa Kitengo cha Damu Salama Mkoa wa Dodoma, Dk. Leah Kitundya alimweleza Waziri Mkuu kwamba Hospitali ya Mkoa wa Dodoma ina upungufu wa damu kwa sababu kuna matukio mengi yanayosababisha upungufu wa damu,

“Tukisema kuwa tunakusanya chupa za kutosha, tunahitaji tuwe na chupa 1,000 hadi 1,500 za damu lakini katika hali ya kawaida huwa tunakusanya chupa za damu 850 hadi 950 tu,” alisema.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com