WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amefanya mazungumzo na mabalozi wa Kenya na Kuwait na kuwasisitizia kwamba Tanzania inakaribisha wawekezaji kutoka kwenye nchi zao na hasa eneo la ujenzi wa viwanda.
Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Aprili 25, 2019) alipokutana kwa nyakati tofauti na Balozi wa Kenya nchini, Bw. Dan Kazungu na Balozi wa Kuwait nchini, Bw. Mubarak Alsehaijan ofisini kwake bungeni jijini Dodoma.
“Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kujenga uchumi wa viwanda, tutafurahi tukipata wawekezaji kutoka Kenya ili waje wawekeze kwenye viwanda kwani tunajua Kenya ilianza mapema kujihusisha na ujenzi wa viwanda wakati sisi tukiwa bado na mfumo wa ujamaa,” amesema.
Waziri Mkuu alimweleza Balozi Kazungu kuwa anatambua kwamba miongoni mwa nchi za Afrika, Kenya inaongoza kwa uwekezaji hapa nchini lakini kwa fursa ambazo Tanzania inazo, bado wanayo nafasi ya kuja kuwekeza.
“Kwa kuzingatia kuwa Mheshimiwa Rais ameleta Waziri, Katibu Mkuu na TIC kwenye ofisi yangu, hii maana yake ninapaswa nisimamie suala la uwekezaji kwa karibu zaidi. Tumetengeneza blueprint, tumeweka taasisi 11 pale TIC za kurahisisha usajili na hivi sasa mwekezaji siyo lazima aje Tanzania, anaweza kujisajili mtandaoni hukohuko aliko,” amesema.
Pia alisisitiiza suala la kulinda amani katika nchi hizo mbili na hasa ulinzi wa mipakani. “Wenzetu mmepata mitisikiko ya ugaidi hivi karibuni, lakini ulinzi wa uhakika wa pamoja ni jambo linalojadilika na linalowezekana. Sisi tuko tayari kuwaunga mkono katika vita dhidi ya ugaidi, uharamia, na usafirishaji wa dawa za kulevya,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Balozi Kazungu amemshukuru Waziri Mkuu kwa ushirikiano ambao Serikali ya Kenya imekuwa ikiupata kutoka Tanzania na kuahidi kudumisha udugu ambao umekuwepo kwa miaka mingi.
“Sisi ni ndugu, tena ni majirani na mtu huwezi kuchagua jirani yako awe nani. Tunahitaji tuwe karibukaribu na kama ni biashara, basi watu wetu wawe wanafanya biashara kama majirani,” alisema Balozi Kazungu.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemshukuru Balozi wa Kuwait kwa misaada ambayo nchi hiyo imekuwa ikiipatia Tanzania kupitia taasisi zake za kijamii.
Mbali na hayo, Waziri Mkuu amesema Serikali ya nchi hiyo kupitia Kuwait Fund, imesaidia ujenzi wa barabara ya Chaya-Nyahua (Tabora), mradi wa maji wa Same - Mwanga - Korogwe na ukarabati wa hospitali ya Mnazi Mmoja huko Zanzibar.
Amesisitiza kuwa bado Tanzania na Kuwait zinahitaji kuimarisha mahusiano yao katika maeneo mengine ya kiuchumi.
Naye Balozi Alsehaijan wa Kuwait amemshukuru Waziri Mkuu na kuahidi kuwa nchi yake iko tayari kuendelea kutoa misaada na huduma za kijamii.
Alisema kupitia taasisi za kujitolea, kuna mashirika manne (charity groups) ambayo yamejenga vituo vya watoto yatima Singida na Mwanza lakini kwa Mwanza, pia wameanza kuwahudumia na watu wenye ulemavu. “Pia wanajenga hospitali huko Zanzibar,” alisema.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,