Mtendaji Mkuu Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, Eng. Peter Ulanga akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo kuhusiana na maadhimisho ya miaka 10 ya mfuko huo yanayofanyika jijini Dodoma yakibebwa na kauli mbiu ya "Mawasiliano kwa Wote ni Kichocheo cha Kuufikia Uchumi wa Kati".
Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote nchini (UCSAF) unatarajia kufanya maadhimisho ya Miaka 10 tangu kuanzishwa kwake. Maadhimisho hayo ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwa Mfuko ni sehemu ya Utekelezaji wa Kauli Mbiu ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Kuufikia Uchumi wa Kati. Kauli mbiu katika maadhimisho haya ni Mawasiliano kwa Wote ni Kichocheo cha Kuufikia Uchumi wa Kati.
Maadhimisho haya yatafanyika hapa Dodoma kuanzia tarehe 27 Aprili hadi kilele chake tarehe 30 Aprili, 2019 ambapo Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mbunge).
Katika maadhimisho haya, Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote umeandaa shughuli mbalimbali katika kipindi cha muda wa maadhimisho, yakiwemo maonesho ya watoa huduma mbalimbali za mawasiliano nchini ambayo yatafanyika kuanzia tarehe 27 Aprili hadi siku ya kilele tarehe 30 Aprili 2019. Mfuko unachukua fursa hii kuualika umma wa wananchi wa Jiji la Dodoma pamoja nanyi waandishi wa habari kuhudhuria maonesho hayo yatakayofanyika kwenye Viwanja vya Mwalimu Nyerere (maarufu kama Nyerere Square) jijini Dodoma.
Sambamba na maonesho hayo, Mfuko utazindua Klabu za TEHAMA katika Shule za Sekondari za Dodoma pamoja na Msalato zilizoko Dodoma siku ya tarehe 28 April 2019. Aidha Mfuko utagawa Kompyuta kwa Wilaya ya Gairo pamoja na kuzindua mnara wa mawasiliano uliopo wilaya ya Bahi siku ya tarehe 29 Aprili 2019, ikiwa ni kielelezo cha miradi ambayo inatekelezwa maeneo mengi nchini Tanzania Bara na Visiwani.
Kwa miongo mingi Sekta ya Mawasiliano imekuwa ikikuwa kwa kasi ndogo katika nyanja zote za simu, posta na utangazaji. Mabadiliko ya Sekta ya Mawasiliano yalianza miaka ya 90 ambapo mfumo wa uendeshaji wa sekta ulibadilishwa na kuingiza uwepo wa wadhibiti wa sekta (Tume ya Mawasiliano na Tume ya Utangazaji) na kuanza kuingiza ushindani katika sekta ya mawasiliano.
Miaka 10 baadaye mabadiliko zaidi ya kisekta yalifanyika kwa kuunganisha Tume ya Mawasiliano na Tume ya Utangazaji na kuunda Mamlaka ya Mawasiliano mwaka 2003. Katika kuongeza ushindani katika soko la mawasiliano lilijitokeza ombwe katika muundo wa sekta katika ngazi ya kiutendaji. Ombwe hilo lilitokana na nguvu za ushindani kujikita kupeleka mawasiliano katika maeneo yenye mvuto wa kibiashara na kuyaacha maeneo ya vijijini na ya mijini yasio na mvuto wa kibiashara.
Serikali ililiona hilo kuanzia mwaka 2003 mpaka mwaka 2006 ambapo sheria ya kuanzisha Mfuko Mahsusi kwa ajili ya Mawasiliano ilipitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mfuko huo ulianzishwa kama taasisi ya serikali inayojitegemea chini ya Wizara inayohusika na mawasiliano. Kanuni za kuanzisha Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote zilisainiwa mwezi Aprili 2009.
Sekta ya Mawasiliano katika kipindi kirefu cha tabribani miaka 30 iliyopita imepitia mabadiliko makubwa sana ambapo sekta imetoka kwenye kuwa na kampuni moja ya umma kabla ya mwaka 1993 ambayo ilikuwa inatoa huduma za simu za mezani, posta na hata telegramu na telex mpaka kuwa na soko kubwa la ushindani lenye makampuni makubwa ya simu za mkononi. Sekta ya mawasiliano imefaidi sana kwa uwepo wa mdhibiti wa mawasiliano aliyethabiti na kutoa mwongozo ambao umeifanya sekta ya mawasiliano kuwa sekta inayochangia maendeleo makubwa ya uchumi wa Tanzania.
Mabadiliko ya kisekta yaliyofanywa na Serikali mwaka 2005 yaliongeza kasi ya ushindani katika sekta ya mawasiliano na mabadiliko ya aina hiyo yalitokea kwenye sekta ya utangazaji na sekta ya posta. Kuongezeka kwa ushindani kulisababisha ushindani wa bei na kufanya gharama kuanza kupungua hata hivyo kutokana na hali hiyo watoa huduma walichelea kupeleka mawasiliano ya aina zote maeneo ambayo yataonekana kukosa mvuto wa kibiashara hasa maeneo ya vijijini.
Serikali ilianzisha Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote mwaka 2006 na kusainiwa na Mheshimiwa Raisi mwaka 2007. Hata hivyo kanuni za kuanzisha Mfuko zilisainiwa Aprili 2009. Lengo kuu la kuanzishwa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ni kuhakikisha Mtanzania popote alipo ataweza kupata huduma za uhakika za mawasiliano iwe ni mawasiliano ya simu za mkononi, utangazaji, huduma za posta au intaneti.
Toka kuanzishwa kwake Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote umejikita kutambua mahitaji ya mawasiliano nchi nzima, kushirikisha wadau mbali mbali wa mawasiliano nchini, kushirikisha wananchi katika kutambua na kutatua kero za mawasiliano. Wakati Mfuko unaanza takriban asilimia 45 tu ya watanzania walikuwa wanaishi katika maeneo yanayofikiwa na mawasiliano ya simu. Mpaka tunavyoongea leo takriban asilimia 94 ya watanzania wanaishi kwenye maeneo yanayofikiwa na mawasiliano ya simu ambapo zaidi ya asilimia 70 ni watumiaji wa huduma za mawasiliano ya simu. Asilimia 10 imechangiwa na Mfuko wa Mawasiliano.
Imetolewa na
Eng. Peter Ulanga
Mtendaji Mkuu
Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote