Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI WA MADINI UGANDA AFURAHISHWA NA USIMAMIZI WA SEKTA YA MADINI NCHINI

Na Greyson Mwase, Geita

Waziri wa Madini Nchini Uganda, Peter Lokeris ames    ema kuwa amefurahishwa na usimamizi wa sekta ya madini nchini Tanzania na kusisitiza kuwa Uganda bado itaendelea kutuma wataalam wake pamoja na wachimbaji wadogo wa madini nchini Tanzania kwa ajili ya kujifunza namna bora ya uchimbaji na uchenjuaji wa madini.

Lokeris aliyasema hayo jana tarehe 02 Aprili, 2019 mara baada ya kutembelea migodi ya wachimbaji wadogo na wa kati ya madini iliyopo Wilayani Geita Mkoani Geita, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku nne nchini Tanzania yenye lengo la kujifunza namna Tanzania ilivyofanikiwa katika Sekta ya Madini kupitia Wizara ya Madini hususan katika kuwasaidia wachimbaji wadogo wa madini.

Akiwa ameongozana na  ujumbe wa maafisa waandamizi kutoka Serikali ya Uganda pamoja na wawakilishi wa wachimbaji wadogo aliwasili mkoani Geita na kupokelewa na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Geita ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Geita pamoja na Naibu Waziri wa Madini Nchini Tanzania, Stanslaus Nyongo.

Ziara hiyo pia ilihusisha wataalam kutoka Wizara ya Madini. Tume ya Madini, vyombo vya ulinzi na usalama vya mkoa pamoja na waandishi wa habari.

Akielezea hali iliyopelekea nchi ya Uganda kuichagua nchi ya Tanzania kama sehemu ya kujifunza kuhusu Sekta ya Madini, Lokeris alisema kuwa, baada ya kutanya  utafiti katika nchi za Aftika Mashariki, walibaini kuwa nchi ya Tanzania ni nchi iliyopiga hatua kubwa kwenye usimamizi wa sheria na kanuni za madini hali iliyopelekea wananchi wengi kunufaika nayo hususan wachimbaji wadogo wa madini.

Aliendelea kusema kuwa, Sekta ya Madini Nchini Uganda ndio inaanza kukua, hivyo wameona ni vyema kuja Tanzania  kwa ajili ya kujifunza na kwenda kuimarisha Sekta ya Madini ili baada ya miaka kadhaa angalau iwe inakaribiana na nchi ya Tanzania.

Akielezea mikakati ya matumizi ya uzoefu mkubwa ujumbe huo ilioupata kutoka kwa nchi ya Tanzania, Waziri Lokeris alisema hatua ya kwanza itakayofanywa na Serikali ya Uganda kupitia Wizara yake ya  Madini ni kuhamasisha wachimbaji wadogo wa madini kuunda vikundi na kuwapatia leseni.

Aliongeza kuwa, mara baada ya kuwapatia leseni hatua itakayofuata itakuwa ni kuwaleta Tanzania kwa ajili ya mafunzo ambapo watajifunza kupitia wachimbaji wadogo wa madini wa Tanzania waliofanikiwa kwenye shugfhuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini.

Aliendelea kueleza kuwa, nia ya Serikali ya Uganda kupitia Wizara yake ya Madini ni kuhakikisha sekta hiyo inakua kwa kasi na kuanza kuzalisha dhahabu na kuuza nyingine nje ya nchi na kujipatia mapato makubwa.

“Tumefurahishwa na usimamizi mzuri kwenye sekta ya madini hususan kwenye eneo la uwezeshaji wa wachimbaji wadogo, tumeona namna wanavyochenjua madini huku wakizingatia sheria na kanuni za mazingira,”alisisitiza Waziri Lokeris.

Naye Naibu Waziri wa Madini Nchini Tanzania, Stanslaus Nyongo akielezea mafanikio ya sekta ya madini nchini alieleza kuwa, mafaniko yaliyopatikana ni pamoja na uboreshaji wa sheria mpya ya madini pamoja na kanuni zake inayotambua madini kama mali ya watanzania na kusisitiza kuwa wachimbaji wadogo wamekuwa wanufaika kwa kiasi kikubwa.

Aliongeza kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Madini imeondoa tozo mbalimbali zisizo za lazima hali iliyopelekea wachimbaji wadogo kuzalisha madini kwa gharama nafuu na kulipa kodi na tozo mbalimbali serikalini.

Alieleza mafanikio mengine kuwa ni pamoja na uanzishwaji wa masoko nchini kama njia mojawapo ya kudhibiti utoroshwaji wa madini kwa kuhakikisha wachimbaji wa madini wanakuwa na soko la uhakika la kuuzia madini yao kwa bei yenye faida.

Naye mmiliki wa mgodi wa  dhahabu wa Blue Reef uliopo katika eneo la Rwamgaza Wilayani Geita mkoani Geita ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Wachimbaji wa Madini Mkoa wa Geita (GEREMA), Christopher Kadeo akizungumza na  ujumbe huo uliofanya ziara kwenye mgodi wake akielezea mchango wa mgodi wake katika jamii iliyopo jirani alisema mgodi wake tangu ulipoanzishwa mwaka 1991 mpaka sasa umefanikiwa kuajiri watumishi 160 na vibarua takribani  200.

Alieleza mafanikio mengine kuwa ni pamoja na uboreshaji wa huduma za jamii kama vile afya, elimu, ulinzi kupitia ujenzi wa vituo vya polisi na kusisitiza kuwa mgodi umekuwa ukishirikiana kwa karibu zaidi na Tasisi nyingine za Serikali kama vile Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Chuo cha Madini Dodoma (MRI), Chuo Cha Ufundi Dar es Salaam (DIT), Wizara ya Madini, Tume ya Madini na mashirika mengine ya kimataifa.

Aidha, aliongeza kuwa mgodi wake umewahi kupewa tuzo ya utunzaji bora wa mazingira na Rais wa Awamu ya Tatu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benjamin Mkapa.

Akielezea mikakati ya mgodi wake kwenye shughuli za uchimbaji wa madini  alisema mgodi wake unatarajia kufanya utafiti zaidi ili kugundua madini zaidi na kuunganisha leseni zake tano unazomiliki na kutoka kwenye uchimbaji wa kati hadi mkubwa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com