Na Amiri kilagalila-Njombe
Wizara ya afya maendeleo ya jamii jinsia wazee na watoto,inatarajia kufikisha bungeni mapendekezo ya muswada wa sheria ya bima ya afya kuwa ni lazima kwa kila Mtanzania.
Hayo yamebainishwa na waziri wa afya maendeleo ya jamii jinsia wazee na watoto Ummy mwalimu,wakati akikagua huduma ya afya inayotolewa katika hospital ya mkoa wa Njombe Kibena.
“Ndani ya mwezi huu nadhani nitapeleka mapendekezo ya muswada wa sheria bungeni ambapo bima ya afya itakuwa ni lazima kwa kila mtanzania mwenye uwezo,nitoe wito kwa wananchi wa Njombe na Tanzania kwa ujumla wajiandae kwa kuwa ili tuweze kupata huduma bora za afya bila kikwazo cha fedha suruhisho ni kuwa na bima ya afya”alisema Ummy mwalimu
Aidha amewataka watoa huduma za afya za serikali kujipanga kuboresha mazingira ya huduma zao ili wateja waweze kuvutiwa na huduma za serikali kama ilivyo katika hospital za binafsi.
Hata hivyo waziri Ummy amesema ameridhishwa na hali ya utoaji huduma za afya katika hospital hiyo huku akikiri uwepo wa upatikanaji wa dawa muhimu katika hospital zote nchini kwa zaidi ya asilimia 90%.
“Kwa kiasi kikubwa hali ya utoaji huduma inaridhisha lakini pia kwa upande wa upatikanaji wa dawa nchini ,tunaposema dawa zinapatikana kwa asilimia 90% sio maneno ya kwenye makaratasi au majukwaani,ninyi wenyewe ni mashahidi na mmeona dawa muhimu zote zinapatikana katika hospital hii na tumehoji wagonjwa dawa mmepata wamesema wanapata vizuri.
"Changamoto kubwa hapa nimebaini kule wodi ya wazazi kuna msongamano mkubwa wa akina mama wajawazito tunaamini hospital mpya ya rufaa ya mkoa wa Njombe itakayowekwa jiwe la msingi na Rais ikikamilika basi changamoto hii itapungua kwa kiasi kikubwa” aliongeza Ummy
Naye katibu mkuu wa wizara ya afya Dkt.Zainab Chaula ameridhishwa na utendaji kazi wa hospital ya mkoa wa Njombe Kibena huku akiwataka watendaji kuwahamasisha wagonjwa wote kuwa na bima ya afya.
“Niombe tuwahamasishe wagonjwa wetu wote wawe na bima ya afya kwa kuwa ukiangalia watumishi wa serikali wote tuna bima na sio kwamba tuna pesa hapana ila ni utaratibu tu uliowekwa na ukiaangalia watumishi ni asilimia 7 tu asilimia 93% ipo nje ya mfumo, hii itatuondolea mgogoro kwasababu wale wenye bima wote wanaenda hospital binafsi wale ambao tunasema hawana uwezo ndio wanakuja huku kwa hiyo tunataka kufanya mabadiliko kila mwenye bima aje hapa mtu awe na uhuru wa kuchagua lakini sio tu kuwa na huduma mbovu”alisema Dkt.Zainab
Winfrid Kiambile ni mganga mfawidhi wa hospital ya rufaa ya mkoa wa Njombe amesema hali ya watumia bima katika hospital hiyo ni nzuri kwa kuwa awali walikuwa wagonjwa 600 kwa mwezi lakini kwa sasa wamefikia 1200 mpaka 1300.
“Kwanza hali ya watoto kufariki kwa sasa imepungua sana ukilinganisha na awali kutokana na maboresho ya mazingira yetu mfano kwa kukarabati jengo la x-ray na kuleta mashine ya kisasa na mambo mengine mengi, lakini pia maambukizi yalisababisha watoto wengi kufariki kwa kweli kwa sasa kwa wiki watoto waliokuwa wakifariki walikuwa ni 12 mpaka 15 tofauti na sasa watoto 3 mpaka 5,kwa upande wa watumiaji bima wameongezeka sana kwa kuwa mwanzo tulianza na 600 na sasa hivi wamefika 1200 mpaka 1300 kwa mwezi”alisema Dkt.kiambile
Baadhi ya wagonjwa waliozungumza na mtandao huu hospitalini hapo wakiwemo akina mama wajawazito wanakiri kuridhishwa na huduma inayotolewa katika hospital ya kibena ikiwemo upatikanaji wa dawa huku wakiomba kuboreshewa upatikanaji wa maji kwani yamekuwa yakikatika mara kwa mara.