YANGA SC YAIGONGESHA KAGERA SUGER 3 - 2 ...YAENDELEA KUBAKI KILELENI


Yanga SC imeendeleza wimbi la ushindi baada ya kuichapa Kagera Sugar mabao 3-2 katika mechi nzuri ya funga nikufunge ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza. 


Ushindi huo unaendelea kuibakiza Yanga kileleni mwa Ligi Kuu, sasa ikifikisha pointi 74 katika mechi ya 31, ikiizidi pointi 11 Azam FC inayofuatia katika nafasi ya pili, wakati mabingwa watetezi, SImba SC ni wa tatu kwa pointi zao 57 za mechi 22.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Alfred Vitalis wa Kilimanjaro aliyesaidiwa na Gasper Ketto wa Arusha na Karume Tawfiq wa Mwanza, hadi mapumziko timu hizo zilikuwa zimefungana 1-1.

Paul Ngwai Ngalyoma alianza kuifungia Kagera Sugar ya kocha Mecky Mexime dakika ya 30 kwa kichwa akimalizia kona nzuri ya Ally Ramadhani ‘Kagawa’.

Yanga SC wakasawazisha bao hilo dakika ya 34, Kassim Hamisi wa Kagera Sugar akipiga fyongo kujifunga wakati akijaribu kuokoa mpira wa kichwa uliopigwa na kiungo Papy Kabamba Tshishimbi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) akimalizia krosi ya beki Gardiel Michael aliyeanzishiwa kona fupi na kiungo Mzimbabwe, Thabani Kamusoko.

Kipindi cha pili Yanga walikianza vizuri na wakafanikiwa kupata bao la pili dakika ya 47 tu, mfungaji mshambuliaji wake tegemeo, Heritier Makambo kutoka DRC aliyemalizia kwa kichwa pasi ndefu ya beki wa kati, Kelvin Yondan, hilo likiwa bao lake la 15 la msimu na sasa anazidiwa moja tu na Salum Aiyee wa Mwadui FC anayeongoza. 

Kassim Hamisi akaisawazishia Kagera Sugar dakika ya 58 akimtungua kipa Mkongo Klaus Kindoki kwa shuti la umbali wa mita 17 baada ya kumlamba chenga beki wa Yanga, Paul Godfrey.

Kiungo Mzimbabwe, Kamusoko akaifungia Yanga bao la ushindi dakika ya 71 baada ya kuanzishiwa mpira wa adhabu na Gardiel Michael na dakika ya 81, Yondan akatolewa kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumpiga kiwiko Kassim Hamisi.

Pamoja na kubaki pungufu, Yanga SC iliendelea kucheza vizuri na kufanikiwa kuulinda ushindi wake ikiendelea kukaa kileleni.

Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Klaus Kindoki, Paulo Godfrey, Gardiel Michael, Kelvin Yondan, Andrew Vincent ‘Dante’, Feisal Salum, Mrisho Ngassa/Mohammed Issa ‘Banka’ dk86, Papy Kabamba Tshishimbi, Heritier Makambo, Thabani Kamusoko na Jaffar Mohammed/Said Juma ‘Makapu’ dk78.

Kagera Sugar; Jeremiah Kisubi, Mwaita Gereza, David Luhende/Japhet Makalai dk85, Juma Shemvuni, Juma Nyosso, Peter Mwalyanzi, Kassim Hamisi, Ally Ramadhani, Omar Mponda/Suleiman Mponda dk60, Paul Ngalyoma na Venence Ludovic.
Chanzo- Binzubeiry blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post