Yanga SC imezinduka baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya African Lyon jioni ya leo Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Ushindi huo wa kwanza katika Ligi Kuu ndani ya mechi tatu, wakitoka kufungwa 1-0 na Lipuli na kutoa sare ya 1-1 na Ndanda FC, zote ugenini unaifanya Yanga SC ifikishe pointi 71 baada ya kucheza mechi 30.
Maana yake, Yanga SC inaendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi 11 zaidi ya Azam FC waliocheza mechi 30 pia wanaofuatia kwenye nafasi ya pili, mbele ya mabingwa watetezi, Simba SC wenye pointi 57 za mechi 22 tu.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Emmanuel Mwandembwa aliyesaidiwa na Ferdinand Chacha na Consolata Lazaro wote wa Mwanza, hadi mapumziko Yanga walikuwa mbele kwa mabao 2-0.
Na yote yalifungwa na mshambuliaji kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Heritier Ebenezer Makambo ambaye yupo katika msimu wake wa kwanza tu tangu asajiliwe kutoka FC Saint Eloi Lupopo ya kwao.
Bao la kwanza alifunga dakika ya tano ya mchezo akimalizia pasi ndefu ya beki wa kati, Kelvin Patrick Yondan na la pili dakika ya 31 kwa kichwa akimalizia mpira wa adhabu wa kiungo Haruna Moshi ‘Boban’.
Kipindi cha pili Yanga SC iliendelea kupeleka mashambulizi langoni mwa African Lyon, lakini ikaishia kukosa mabao ya wazi mfululizo.
Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Klaus Kindoki, Juma Abdul, Gardiel Michael, Andrew Vincent ‘Dante’, Kelvin Yondan/Said Juma ‘Makapu’ dk52, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Mrisho Ngassa/Raphael Daudi dk85, Haruna Moshi ‘Boban’/Thabani Kamusoko dk73, Heritier Makambo, Papy Kabamba Tshishimbi na Pius Buswita.
African Lyon; Douglas Kisembo, Khalfan Mbarouk, Kassim Simbaulanga, Baraka Jaffary, Daudi Mbweni, Jabir Aziz, Said Mtikila, Awadh Juma, Benedictor Jacob/Adil Nassor dk46, Kassim Mdoe na Hamisi Thabiti.
Chanzo - Binzubeiry
Social Plugin