Chama cha ACT Wazalendo kimewapongeza Mwanaharakati Bob Chacha Wangwe, Wakili Fatma Karume na Wanaharakati wote ambao walishiriki katika kufungua kesi ya kupinga Wakurugenzi wa Halmashauri za Miji, Wilaya na Majiji kutumiwa na Tume ya Uchaguzi (NEC) kama wasimamizi wa uchaguzi mkuu.
Katibu Mwenezi wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu amesema kuwa historia ya Tanzania itawakumbuka wanaharakati hao walioshiriki kwenye kesi hiyo kwa sababu itaacha alama ya kudumu kwenye historia ya mapambano ya haki, demokrasia na ustawi wa taifa.
"Ingawa ni utekelezaji wa kawaida wa majukumu yao na isingetazamiwa wasifiwe, ACT Wazalendo kinawapongeza majaji Mh. Jaji Dk. Atuganile Ngwala, Mh. Jaji Benhaj Masoud na Mh. Jaji Firmin Matogolo kwa kusimamia haki bila kuyumba kwenye shauri hili," amesema Ado.
Utakumbuka Mei 10 mwaka huu Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, ilitoa uamuzi kuhusu Shauri la Kikatiba namba 17 la mwaka 2018 lililofunguliwa na Bob Chacha Wangwe kupinga baadhi ya vifungu vua Sheria ya Taifa ya Uchaguzi vinavyohusu Wasimamizi wa Uchaguzi kuwa vinakinzana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kama ilivyofanyiwa marekebisho.
Shauri hilo lilifunguliwa dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Tume ya Taifa yaUchaguzi na Mkurugenzi wa Uchaguzi.
Hata hivyo, hapo jana Serikali imewasilisha notisi Mahakama ya Rufaa kupinga sehemu ya uamuzi wa Mahakama Kuu katika kesi ya Kikatiba iliyofunguliwa na Bob Chacha Wangwe dhidi Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wenzake kupinga baadhi ya vifungu vya Sheria ya Taifa Uchaguzi kuhusu Wasimamizi wa Uchaguzi.
Social Plugin