Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

AGPAHI YAADHIMISHA SIKU YA MKUNGA DUNIANI KWA KUCHUNGUZA SARATANI YA MLANGO WA KIZAZI KWA AKINA MAMA


Shirika lisilokuwa la kiserikali Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI) limeshiriki maadhimisho ya siku ya mkunga duniani kwa kutoa huduma ya uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi kwa akina mama pamoja na upimaji wa Virusi Vya Ukimwi (VVU) mkoani Simiyu.



Maadhimisho hayo  kitaifa yamefanyika leo Mei 5, 2019 kwenye uwanja wa michezo wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu ambapo mgeni rasmi alikuwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt Faustine Ndugulile akimwakilisha Makamu wa Rais,Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Mratibu wa Shirika la AGPAHI mkoa wa Simiyu Dafrosa Charles,alisema shirika la AGPAHI limeshiriki maadhimisho ya siku ya mkunga duniani kwa kutoa huduma ya uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi kwa akina mama pamoja na upimaji wa Virusi Vya Ukimwi (VVU).

Amesema kati ya akina mama 205 waliowafanyia uchunguzi wa saratani hiyo ya mlango wa kizazi, wawili waligundulika kuwa na tatizo hilo na wamepatiwa rufaa ya kwenda kutibiwa kwenye hospitali ya rufaa Bugando Jijini Mwanza, huku 166 waliowapima VVU, mmoja kati yao amebainika kuwa ana maambukizi ya VVU na ameanzishia huduma ya dawa za kupunguza makali ya VVU.

Aliongeza kuwa Saratani hiyo ya mlango wa kizazi kwa sasa ndiyo imekuwa ikisababisha vifo vingi vya akina mama wakati wa kujifungua kutokana na kuvuja damu kwa wingi na kuwataka akina mama wajenge tabia ya kupima afya zao mara kwa mara ili waweze kupata matibabu mapema na ili kumaliza vifo hivyo.

Baadhi ya akina mama waliopatiwa huduma kwenye banda la Shirika la AGPAHI akiwemo Pendo Mboje, wamelipongeza Shirika hilo kwa kuwapelekea huduma hiyo, ambapo walikuwa hawajui visababishi vya kuugua saratani ya mlango wa kizazi pamoja na athari zake na kuahidi kujilinda zaidi na kwenda kutoa elimu kwa wenzao.

Maadhimisho hayo ya siku ya mkunga dunia kitaifa hapa nchini yamefayika mkoani Simiyu yakiwa na kaulimbiu isemayo,”Wakunga watetezi wa haki za wanawake”.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Faustine Ndugulile alimewataka wakunga kuendelea kutoa huduma nzuri kwa akina mama wajawazito na kuwaasa kuacha tabia ya kuwatolea lugha chafu ili kuongeza idadi kubwa ya wanawake kupenda kujifungulia kwenye vituo vya afya hali ambayo itapunguza tatizo la vifo vitokanavyo na uzazi.

“Licha ya Serikali kupunguza tatizo la vifo vya mama na mtoto vitokanavyo na uzazi bado hali siyo ya kuridhisha ambapo awamu hii ya tano tumedhamiria kabisa kumaliza changamoto hiyo kwa kuhakikisha tunaendelea kuboresha huduma za afya hasa za mama na mtoto,”aliongeza.


Rais wa Chama cha Wakunga Tanzania (TAMA) Feddy Mwanga, alisema kilianzishwa mwaka 1992 kwa lengo la kuunganisha wakunga wasajiliwa nchini ili kuwa na nguvu moja katika kupambana kumaliza tatizo la vifo vya mama na mtoto vitokanavyo na uzazi wakati wa kujifugua.

“Hapa mkoani Simiyu Chama cha Wakunga Tanzania kimeadhimisha siku hii kuanzia Mei 3 hadi leo Mei 5,2019 kwa kushirikiana na wadau wenzetu ambao wametoa huduma mbalimbali za afya ukiwamo upimaji wa VVU, huduma za uzazi wa mpango na uchuguzi wa saratani ya mlango wa kizazi na matiti,”alisema Mwanga.

Naye katibu tawala wa mkoa wa Simiyu Jumanne Sagini alisema takwimu za vifo vya mama na mtoto vitokanavyo na uzazi kuwa vimepungua ambapo mwaka 2017 vilikuwa 48 ambapo mwaka 2018 vilitokea vifo 40 na kubainisha kuwa tatizo ni kuwapo kwa upungufu wa wakunga .
ANGALIA PICHA


Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,Faustine Ndugulile akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya mkunga duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani Simiyu na kuwataka wakunga kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na kuacha lugha za matusi kwa wajawazito ili kuhamasisha kujifungulia kwenye huduma za kiafya na ili kumaliza vifo vitokanavyo na uzazi.Picha na Marco Maduhu- Malunde 1 blog

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt Faustine Ndugulile (wa pili kulia) akiwa na viongozi wa mkoa wa Simiyu kwenda kukagua mabanda ya wadau wa sekta ya afya likiwemo shirika la AGPAHI ambao wametoa huduma mbalimbali za kiafya kwenye maadhimisho hayo ya siku ya mkunga duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani Simiyu.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt Faustine Ndugulile akiwa kwenye banda la Shirika la AGPAHI akipewa maelezo na Mratibu wa AGPAHI mkoa Simiyu Dafrosa Chalres namna linavyotoa huduma ya uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi kwa akina mama pamoja na kuwapima maambukizi ya VVU na kuanza kuwapatia huduma wale ambao wanagundulika kuwa na magonjwa hayo.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt Faustine Ndugulile , akipokea kijizuu kwenye banda la Shirika la AGPAHI.

Muuguzi mkunga Conchesta Alexander kutoka kituo cha afya Muungano Bariadi mkoani Simiyu, akitoa elimu kwa akina mama mkoani humo juu ya kujikinga na saratani ya mlango wa kizazi ugonjwa ambao unaua akina mama wengi wakati wa kujifungua.

Muunguzi mkunga kutoka kituo cha afya muungano Bariadi , Elizabeth Holela akitoa elimu kwa akina mama juu ya saratani ya mlango wa kizazi, madhara yake pamoja na namna ya kujikinga.

Muuguzi mkunga kutoka hospitali ya mkoa wa Simiyu Conchesta Alexander akiendelea kutoa elimu kwa akina mama mkoani humo kwenye Banda la AGPAHI namna ya kujiepusha na magonjwa ya saratani ya mlango wa kizazi.

Akina mama mkoani Simiyu wakiwa kwenye Banda la Shirika la AAGPAHI kupewa elimu ya saratani ya mlango wa kizazi, ili kutokomeza vifo vya mama na mtoto vitokanavyo na uzazi.

Akina mama mkoani Simiyu wakiwa kwenye Banda la Shirika la AGPAHI kupewa elimu ya saratani ya mlango wa kizazi, ili kutokomeza vifo vya mama na mtoto vitokanavyo na uzazi.

Mratibu wa Shirika la AGPAHI mkoani Simiyu Dafrosa Charles akitoa elimu kwa mmoja wa wanaume mkoani Simiyu namna ya kumkinga mke wake kutopata saratani ya mlango wa kizazi.

Muuguzi mkunga Mwaisha Yoma kutoka kituo cha afya Muungano Bariadi akichukua maelezo kwa mmoja wa akina mama ambaye amejitokeza kufanyiwa uchuguzi wa saratani ya mlango wa kizazi kutoka kwenye Banda la AGPAHI.

Pendo Mbonje ambaye ni mmoja wa akina mama mkoani Simiyu ambao wamejitokeza kufanyiwa uchunguzi wa Saratani ya mlango wa kizazi katika banda la AGPAHI, wakati wa maadhimisho ya ukunga duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani humo Simiyu.

Seke Ndongo akielezea namna alivyofanyiwa uchuguzi wa Saratani ya mlango wa kizazi na alivyopewa elimu ya kujikinga na saratani hiyo.




Katibu tawala wa mkoa wa Simiyu Jummane Sagini akiiomba wiraza ya afya impatie wauguzi wakunga ili kukabiliana na tatizo la vifo vya uzazi mkoani humo, ambapo kwa mwaka jana walipoteza maisha akina mama 40.

Rais wa Chama cha Wakunga Tanzania Feddy Mwanga akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya mkunga duniani kitaifa mkoani Simiyu, na kuelezea malengo ya maadhimisho hayo kufanyika mkoani Simiyu kuwa ni kuunganisha nguvu za pamoja kupambana kumaliza tatizo la vifo vya mama na mtoto vitokanavyo na uzazi.

Wakunga wakiwa kwenye maadhimisho yao kitaifa mkoani Simiyu wakisikiliza nasaha za Naibu waziri wa afya ,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Faustine Ndugulile namna ya kuzingatia maadili ya kazi yao kiufasaha ili kutokomeza vifo vya uzazi.

Wananchi mkoani Simiyu wakiwa kwenye maadhimisho ya siku ya mkunga duniani mkoani humo.

Awali naibu waziri wa afya maendeleo ya jamiim jinsia wazee na watoto Dkt Faustine Ndugulile mwenye kaunda suti akipokea maandamano ya wakunga kwenye maadhimisho hayo kitaifa mkoani Simiyu.

Wakunga wakiingia kwa maandamano kwenye uwanja wa michezo wa halmashauri ya mji wa Bariadi wakitokea kwenye kituo cha afya cha Muungano mjini Bariadi.

Wauguzi wakunga nao hawakuwa nyuma kutoa burudani kwenye maadhimisho yao ya siku ya mkunga duniani, yaliyofanyika kitaifa mkoani Simiyu.

Wakunga wakiendelea kutoa burudani.
Picha na Marco Maduhu- Malunde 1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com