Polisi jijini Mwanza imemkamata askari magereza Kibemba Warioba (27) mwenye namba za usajili B.9205 WDR, akiwa na simu tano za aina tofauti na mitandao tofauti akijihusisha na makosa ya kujipatia pesa kwa njia ya udanganyifu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro amesema kuwa tukio hilo limetokea juzi saa nne na nusu asubuhi, ambapo polisi wa mkoa wa Mwanza kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi la Mkoa wa Kagera walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo ambaye alikuwa anafanya kazi wilayani Biharamulo mkoani Kagera na tayari amesimamishwa kazi kwa hatua zaidi za kisheria.
Kamanda Muliro alisema polisi walimbaini mtuhumiwa huyo akitumia njia ya mitandao hiyo ya simu ambapo alianzisha Saccos ‘Bandia,’ iliyojulikana kwa jina la Info Tell CCM, akilenga kuwatapeli wanachama wa CCM na wengine katika mikoa ya Mara na Kagera.
Alitoa onyo kwa wananchi wenye tabia ya kufanya vitendo hivyo vya uhalifu waache mara moja kwa kuwa ni kinyume cha sheria.
Social Plugin