Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zachary Kakobe, ameibuka katika Kanisa la Ufufuo na Uzima linaloongozwa na Askofu Josephat Gwajima na kukanusha kuwa video za ngono zinazosambaa mitandaoni zikimuonyesha Askofu huyo kuwa si za kweli.
Akizungumza katika ibada iliyofanyika katika kanisa hilo leo Jumapili Mei 12, Kakobe amesema vitabu vya dini haviamini ushahidi wa picha isipokuwa mashahidi watakaozungumza juu ya ukweli wa tukio husika.
“Yuko wapi huyo mshitaki mpaka sasa, mbona hayupo amefutika na kama hayupo huo tunauita unafiki, mshitaki wa Gwajima yuko wapi ? Polisi ndio wanamtafuta sasa hivi, sasa kama una ushahidi wa halali kwanini unajificha.
“Hatukubali Mashitaka juu ya Askofu Gwajima isipokuwa kwa vinywa vya mashahidi wawili watatu watakaosimama na kuthibitisha juu ya video ile,” amesema Askofu Kakobe.
Aidha, Kakobe amesema neno alilolitoa Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima katika sherehe za kanisa lake kutimiza miaka 30 alijua litakuwa na majibu.
Kakobe amesema wengi walichukia kwa nini Makonda alialikwa katika sherehe hizo na wengine walichukia zaidi baada ya Gwajima kukumbatiana na mkuu huyo wa mkoa huku wakibaki kutega masikio leo wakisubiri kuanzisha awamu ya pili ya mafarakano jambo ambalo halipo.
“Kwa neno alilolitoa Gwajima lilikuwa limejaa upako nilijua tu kuna kitu lazima kitokee na kama isingekuwa hivyo basi shetani angekuwa amekufa,” amesema Kakobe.
Amesema shetani hapendi kuona watu wakiwa wamoja na ndiyo maana hujaribu kuwatawanya ili iwe rahisi kuwatawala.
“Mshikamano huu wa wachungaji na manabii shetani wa kuubomoa bado hajazaliwa kwa sababu shetani anajua mkiwa wamoja katika kristo, baraka za Mungu ndiyo zinapowajia,” amesema Kakobe.
Social Plugin