Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeitaka Serikali na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuanza kujipanga kutekeleza uamuzi wa Mahakama Kuu kuhusu wakurugenzi kusimamia uchaguzi.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema, alisema hukumu hiyo itasaidia kutengeneza uwanja sawa wa wapigakura.
“Hatutegemei CCM na serikali yake wakate rufaa kwa lengo la kutuchelewesha, tunaamini wataheshimu uamuzi wa mahakama tutengeneze uwanja sawa wa wapigakura ili kila mtu ashinde kwa usawa,” alisema Mrema.
Chama hicho kilidai kuna wakurugenzi 86 ambao ni makada wa CCM kinyume na Ibara ya 74 (14) ya Katiba ambayo inapiga marufuku mtu anayehusika na uchaguzi kuwa mwanachama wa chama cha siasa.
“Mahakama Kuu imeona na kwa ushahidi kuna makada katika halmashauri 86 ambao walikuwa wanasimamia uchaguzi kinyume na Katiba.
“Wengi waligombea mwaka 2015 wakashindwa kwenye majimbo na kata na wengine walishindwa kura za maoni. Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unasimamiwa na makatibu tawala na wengi ni makada wa CCM, tunaomba washeshimu uamuzi wa Mahakama Kuu,” alisema.
Chama hicho pia kilipendekeza iundwe tume huru ya uchaguzi na uwepo utaratibu wa kuwapata makamishna wa tume sambamba na kuwa na mfuko maalumu ili ifanye kazi kwa uhuru.
“Kenya, Malawi na nchi zingine watu huwa wanaomba hiyo kazi ya ukamishna na si kuteuliwa, na zuio la kuishtaki tume liondolewe,” alisema Mrema.
Kwa mujibu wa Mrema, pendekezo lingine ni haki ya mgombea kukata rufaa pale ambapo wasimamizi wa uchaguzi wanakataa kupokea fomu au wanaondoka ofisini.
Chadema kilipendekeza pia wananchi wapewe fursa za kupiga kura za ndio au hapana iwapo mgombea atapita bila kupingwa na kama ikitokea hatavuka asilimia 50 asitangazwe mshindi.
Wiki iliyopita Mahakama Kuu ilibatilisha vifungu vya Sheria ya Uchaguzi vinavyowapa mamlaka wakurugenzi wa halmashauri za majiji, miji, wilaya na manispaa kuwa wasimamizi wa uchaguzi kwa niaba ya NEC.
Social Plugin