Chama tawala cha Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ANC kitahifadhi wingi wake wa viti bungeni baada ya uchaguzi, ijapokuwa umaarufu wake utapungua na hivyo kuathiri jitihada za kukifufua chama hicho na pamoja na uchumi unaoyumba wa nchi hiyo.
African National Congress, ambacho kimekuwa madarakani tangu 1994, kinaendelea kuongoza kikiwa na karibu asilimia 57 ya kura baada ya zaidi ya nusu ya maeneo ya kupigia kura kuhesabiwa rasmi kufuatia uchaguzi wa Jumatano.
Ramaphosa mwenye umri wa miaka 66, alichukua usukani mwaka jana baada ya chama hicho kumlazimu aliyekuwa rais wakati huo Jacob Zuma kujiuzulu baada ya miaka tisa iliyozongwa na madai ya rushwa na matatizo ya kiuchumi.
Matokeo yaliyotolewa na tume ya uchaguzi yanaonyesha kuwa mpinzani wa karibu kabisa wa ANC, chama kikuu cha upinzani cha Democratic Alliance - DA kinafuata na asilimia 23. Chama cha Economic Freedom Fighters kikiongozwa na Julius Malema ni cha tatu na asilimia 10.
Matokeo rasmi yanatarajiwa kutolewa Jumamosi.