Na Bakari Chijumba, Lindi.
Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa Mkoani Lindi, Hashim Mgandilwa amepiga marufuku wamiliki wa viwanja vya kucheza unyago kutumia Mangariba wasio na vitambulisho vya wajasiriamali wadogo.
Amesema hayo 23 Mei 2019, wakati wa kikao cha mangariba(Wanaotahiri watoto), waganga wajadi na wamiliki wa viwanja vya kuchezea unyago kilichofanyika ukumbi wa CCM Ruangwa mjini.
Mgandilwa amemtaka kila waganga wa jadi kuwa na kitambulisho cha mjasiriamali mdogo kama anataka kuendelea kutoa tiba katika Wilaya ya Ruangwa.
Mkuu huyo wa wilaya amesema wamiliki wa viwanja vya unyago wanapaswa kuzingatia ratiba ya kufunga na kufungua shule ili mtoto anafanyiwa unyago asikose haki ya kupata elimu.
"Msitafute shida,Halmashauri ikianza kutoa vibali vya sherehe hizo nitafuatilia kama umepokea watoto siku husika ya tarehe 8 mwezi wa 6 na kumaliza tarehe 6 mwezi wa 7 ikifika tarehe ya mwisho watoto wote wawe wametoka Jando" amesema Mgandilwa.
Aidha Mgandilwa amewataka wazazi na wahusika wa shughuli za unyago, kuhakikisha watoto wanapokuwa jandoni wanalazwa kwenye vyandarua ili kuepusha maradhi na pia amesisitiza umuhimu kuzingatia usafi wa maeneo ya viwanja vya unyago.
"Mnapofanya shughuli hizi zingatieni msingi ya afya kila mwenye kiwanja awe na uhakika na daktari ni vyema tukaangalia usalama wa watoto wetu" amesema Mgandilwa
Mgandilwa amewataka pia wanaohusika na shughulia za jando, kuzingatia mafunzo wanayotoa kwenye jando na unyago yaendane na maadili ya kitanzania na umri wa watoto wanaopewa hayo mafunzo.
Social Plugin