Dhana ya Afya moja ambayo hujikita katika kujumuisha sekta zote za Afya katika kujiandaa, kufuatilia na kukabili magonjwa yanayomuathiri binadamu imeendelea kufundishwa kwa Wataalamu wa sekta hizo za Afya, ikiwa ni Sekta ya Afya ya Binadamu, Wanyamapori, Mifugo, Kilimo na Mazingira, ili wataalamu hao watumie dhana hiyo kuimarisha udhibiti wa magonjwa ambukizi kati ya Binadamu na wanyama ambayo hutokea mara kwa mara katika maeneo ya mipakani kutokana na kuwepo kwa mwingiliano mkubwa kati ya watu na wanyama katika mazingira yao.
Pamoja na Mwingiliano huo wenye faida kubwa kiuchumi lakini pia unasababisha kuenea kwa vimelea kwa uharaka zaidi na kusababisha magonjwa kwa binadamu, wanyama na mimea katika mazingira yao, hivyo ili kuimarisha Afya ya binadamu, Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), pamoja na watalaamu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine wamewapa mafunzo wataalamu wa sekta za Afya wanao toka katika Halmashauri za Mkoa wa Mbeya na Songwe zilizo mipakani juu ya namna ya kujiandaa na kukabili magonjwa ambukizi kama vile Ugonjwa wa Kimeta kwa kutumia Dhana ya Afya moja.
Akiongea wakati wa kufunga mafunzo hayo yaliyofanyika kuanzia tarehe 29 Aprili hadi,tarehe 3 Mei, 2019, Mkoani Songwe, Mkurugenzi wa Uratibu Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe, ambaye aliwakilishwa na Mratibu Kitaifa, Dawati la Kuratibu Afya Moja, Ofisi ya Waziri Mkuu, Harrison Chinyuka, alibainisha kuwa ushirikiano wa wataalam na sekta za Afya kwa kutumia dhana ya Afya Moja hivi sasa ni agenda ya dunia nzima. Aidha, alieleza kuwa Dhana hiyo imekusudiwa kutumika maeneo ya mipakani ambapo mwingiliano huo huchochewa na wasafiri kutoka eneo moja kwenda jingine, ongezeko la watu duniani, mabadiliko ya tabia nchi, utandawazi, ongezeko la mahitaji ya maji na chakula.
Awali akiongea katika mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo nchini, Dkt. Hezron Nonga alibainisha kuwa sekta za Afya zikishirikiana katika Kudhibiti magojwa zitasaidia kuimarisha Afya ya Binadamu kwa kuwa kila sekta itakuwa inachukuwa tahadhri kwa wakati. Aidha alibainisha kuwa vimelea vingi vinavyo sabababisha magonjwa kwa binadamu asilimia (60%) vinatoka kwa wanyama pori na mifugo na maambukizi yanatokea pale binadamu anapoingilia maskani ya wanyama hao bila tahadhari, hivyo Afya moja ikitumika maeneo ya mipakani itasaidia kuimarisha udhibiti wa magonjwa ambukizi yanayotokana na shughuli za mwingiliano wa wanyama na binadamu zinazofanyika sana maeneo ya mipakani.
Katika kuhakikisha watalaam hao kutoka sekta za Afya wanaweza kutumia Dhana hiyo katika kudhibiti magonjwa katika maeneo ya mipakani wameweza kujengewa uwezo wa namna ya kutoa taarifa za milipuko ya magonjwa ambukizi kama vile ugonjwa wa Kimeta, pindi unapotokea maeneo ya mipakani, Namna ya kuunda vikosi vya kufuatilia na kukabili Ugonjwa, Mawasiliano wakati wa kufuatilia na kukabili magonjwa hayo kwa kutumia Dhana ya Afya moja, pamoja na masuala ya kutumia vifaa Kinga Binafsi vya Kitaalamu.
Tarehe 13 Februari 2018, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa alizindua Dawati la Uratibu la Afya moja chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, likiwa na lengo la kusimamia na kuratibu shughuli za Afya moja nchini. Kwa kutambua umuhimu huo Idara ya Uratibu Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, kupitia Dawati la Uratibu wa Afya moja kwa kushirikiana Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) waliandaa na kuratibu mafuzo hayo.
Social Plugin