Serikali imesema inamalizia kuandaa utaratibu kupitia Benki Kuu (BoT), ikiwemo uhakiki wa taarifa za maduka ya kubadilishia fedha za kigeni yaliyofungiwa ili kuweza kutoa vibali maalumu kwa maduka hayo kuendelea na biashara hiyo.
Pia imesisitiza utawala bora katika taasisi za kifedha ikiwemo benki kwani ndiyo msingi wa maendeleo na katika kipindi cha mwaka jana benki tano zilifungwa baada ya kufilisika na kusababisha hasara kwa wateja, wawekezaji, wadau mbalimbali na wanahisa.
Kauli hiyo ilitolewa juzi jijini Arusha na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alipokuwa akifungua semina ya wanahisa wa Benki ya CRDB, iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa AICC, kabla ya kufanyika kwa mkutano mkuu wa 24 unaotarajiwa kufanyika leo.
Alisema Serikali imefanya jitihada za kuratibu mfumo wa udhibiti wa matumizi ya fedha za kigeni unaolenga kuondoa biashara ya dola kiholela na kuwa wameanza na benki kupata vibali vya kubadili fedha za kigeni na kuwa baada ya uhakiki watatoa fursa kwa wafanyabiashara mmoja mmoja wa maeneo mbalimbali ya kimkakati nchini.
“Tumeanza na mabenki baada ya uhakiki unaoendelea tunaweza tukatoa fursa kwa wafanyabiashara mmoja mmoja wa maeneo ya kimkakati ili kuwa na maduka tunayoyafahamu, yaliyosajiliwa vizuri yanayoweza kufanya biashara hii vizuri kuliko ambavyo ilikuwa awali.
“Niseme hata kwa wale ambao walikuwa wanafanya biashara hiyo na shughuli zao kwa sasa zimesimama, BoT inakamilisha uratibu wao na mawasiliano yao na wateja wao ili baadaye kwa utaratibu mzuri wa kutoa vibali vya uendeshaji wa maduka hayo kwa hiyo wale wote ambao walikuwa na maduka wasiwe na mashaka taratibu zinaendelea.
“Lakini kwa sasa CRDB ni miongoni mwa benki na inaongoza kufanya biashara ya kubadili fedha, nawapongeza kwa mikakati mbalimbali mnayoweka ikiwemo ya kushiriki shughuli ambazo Serikali yetu inafanya na yanayoleta tija kiukweli mmetufikisha pazuri,” alisema.
Social Plugin