1.0 UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba, kufuatia taarifa iliyowasilishwa leo na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo Mifugo na Maji, Bunge lako Tukufu sasa lipokee na kujadili taarifa ya utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka wa fedha 2018/2019. Aidha, ninaliomba Bunge lako Tukufu lipitishe Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara na Taasisi zake kwa mwaka wa Fedha 2019/2020.
2. Mheshimiwa Spika, awali ya yote ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kufikia siku ya leo tukiwa wazima wa afya njema na kuendelea kuijalia nchi yetu amani na mshikamano na kujadili bajeti hii inayolenga kusukuma mbele kasi ya maendeleo ya Sekta ya Kilimo na wakulima kwa ujumla wao.
3. Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru kwa dhati Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuniteua kuwa Waziri wa Kilimo. Pia, niwashukuru Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais na Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.), Waziri Mkuu kwa kazi kubwa wanayofanya kusukuma maendeleo ya nchi hii, ikiwemo Sekta ya Kilimo. Napenda kuwaahidi kwamba nitafanya kazi ya kuongoza Wizara ya Kilimo kwa uaminifu, juhudi na maarifa ili kuhakikisha kuwa rasilimali zinazotengwa kwa ajili ya maendeleo ya kilimo zinawafikia walengwa ili kuongeza tija na kuinua kipato chao.
4. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kumpongeza Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.) kwa hotuba yake ambayo iligusa maeneo mengi ikiwemo Sekta ya Kilimo. Aidha, nimpongeze tena Mhe. Waziri Mkuu kwa kuendelea kuwa mstari wa mbele kuhamasisha na kusimamia kilimo pamoja na maendeleo ya Vyama vya Ushirika.
5. Mheshimiwa Spika, napenda kukupongeza wewe na Naibu Spika Mhe. Dkt. Tulia Ackson Mwansasu (Mb.) pamoja na Wenyeviti wa Bunge kwa jinsi mnavyoliongoza Bunge kwa umahiri mkubwa.
Aidha, nitumie nafasi hii kuwapongeza Wabunge wote kwa umahiri wao mkubwa katika mijadala inayoendelea katika Bunge hili la Bajeti.
6. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia kuwapongeza na kuwashukuru wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo Mifugo na Maji chini ya Uenyekiti wa Mhe. Mahmoud Mgimwa, Mbunge wa Mufindi Kaskazini na Makamu Mwenyekiti Mhe. Dkt. Christine G. Ishengoma (Mb). Kamati ilipata fursa ya kukutana na Wizara na kutembelea baadhi ya maeneo kuona utekelezaji wa kazi za kilimo na kushauri namna ya kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya Wizara, Bodi na Taasisi zake. Naomba kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba, ushauri wao umezingatiwa na tutaendelea kushirikiana na Kamati ili kuleta mageuzi ya kilimo nchini.
2.0 MWELEKEO WA SEKTA YA KILIMO
7. Mheshimiwa Spika, Serikali imepanga kubadilisha kilimo kutoka kuwa cha kujikimu na kuwa kilimo cha kibiashara kama ilivyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025. Aidha, Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo umesisitizia mapinduzi ya viwanda na umeitambua Sekta ya Kilimo kuwa mhimili imara kwa ajili ya upatikanaji wa malighafi za viwanda. Miongozo hiyo ya Kitaifa, pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 na Sera ya Kilimo ya mwaka 2013, inatekelezwa na Wizara kupitia Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) ambayo inalenga kuleta mageuzi katika Sekta ya Kilimo. Aidha, kwa kutambua umuhimu wa kuongeza mitaji, teknolojia na ubunifu, Sekta Binafsi inashirikishwa kikamilifu katika utekelezaji wa ASDP II.
8. Mheshimiwa Spika, ASDP II iliyozinduliwa rasmi tarehe 4 Juni, 2018 na Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inalenga kubadilisha maisha ya mkulima kwa kufanya mageuzi makubwa kwenye kilimo kwa kuzingatia mazao ya kipaumbele kulingana na ikolojia za kilimo.
3.0 MCHANGO WA KILIMO KATIKA UCHUMI
9. Mheshimiwa Spika, kilimo ni sekta kubwa na muhimu kwa maendeleo kutokana na mchango wake katika uchumi. Katika mwaka 2017, sekta hiyo imetoa ajira kwa Watanzania kwa asilimia 65.5, ikichangia takriban asilimia 28.7 ya Pato la Taifa ambapo sekta ndogo ya mazao ilichangia asilimia 16.58. Vilevile, Sekta ya Kilimo inachangia asilimia 65 ya malighafi za viwanda. Takwimu zinaonesha kuwa katika robo ya kwanza ya mwaka 2018, ukuaji wa Sekta ya Kilimo ulifikia asilimia 7.1. Ukuaji huo ulichangiwa na jitihada za Serikali za kuhakikisha upatikanaji na matumizi ya pembejeo bora, hali nzuri ya mvua na uboreshaji wa miundombinu ya uzalishaji.
3.1 Upatikanaji wa Chakula
10. Mheshimiwa Spika, upatikanaji wa chakula kwa mwaka 2018/2019 ulifikia tani milioni 16.89 zikiwemo tani milioni 9.53 za mazao ya nafaka na tani milioni 7.35 za mazao yasiyo nafaka. Kiwango hicho cha uzalishaji kimeiwezesha nchi kujitosheleza kwa mahitaji yake ya chakula ya tani milioni 13.56 na hivyo kuwa na ziada ya tani milioni 3.32 za chakula kwa kiwango cha utoshelevu cha asilimia 124. Niwahakikishie watanzania kwamba, tunacho chakula cha kutosha nchini. Hata hivyo, tuendelee kuweka akiba katika kaya zetu hadi tutakapovuna tena kwani inaonekana kwamba huenda tusiwe na mavuno mazuri sana msimu huu kutokana na uhaba wa mvua kwenye maeneo ya Kanda ya Ziwa, Kati na Kaskazini mwa nchi yetu.(Maelezo ya kina yanapatikana uk.5 wa kitabu cha Hotuba ya bajeti).
3.2 Umwagiliaji
11. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/2019, Wizara kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imekamilisha mapitio ya Mpango Kabambe wa Taifa wa Umwagiliaji wa mwaka 2002 ili kubaini maeneo yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji kwa kuzingatia Mipango Shirikishi ya Maendeleo ya Rasilimali za Maji. Katika mpango huo, hekta 560,880 zimepangwa kuendelezwa kwa lengo la kuongeza eneo la umwagiliaji kutoka hekta 475,052 mwaka 2018/2019 hadi hekta 1,000,000 ifikapo mwaka 2035. (Maelezo ya kina yanapatikana uk.6 wa kitabu cha Hotuba ya bajeti)
3.3 Maendeleo ya Ushirika
12. Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika imeendelea kuimarisha Sekta ya Ushirika kwa kusimamia na kuhamasisha maendeleo yake. Vyama vya Ushirika vimeongezeka kutoka vyama 10,990 Desemba 2017 hadi vyama 11,331 kufikia Desemba 2018. Vilevile, idadi ya wanachama wa vyama vya ushirika imeongezeka kutoka 2,619,311 mwaka 2017 hadi 3,998,193 Februari, 2019 sawa na ongezeko la asilimia 53.
Hadi Desemba 2018, mikopo yenye thamani ya Shilingi trilioni 1.3 imetolewa kwa wanachama ikilinganishwa na Shilingi bilioni 902 iliyotolewa kufikia Desemba 2017.
Aidha, Akiba na Amana za wanachama katika SACCOS zimefikia Shilingi bilioni 575 na hisa Shilingi bilioni 79. (Maelezo ya kina yanapatikana uk.7 wa kitabu cha Hotuba ya bajeti)
4.0 UTEKELEZAJI WA MAENEO YA KIPAUMBELE KWA MWAKA 2018/2019
13. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/2019, Wizara imetekeleza maeneo ya kipaumbele ya kuongeza tija kwa kuimarisha upatikanaji wa pembejeo za kilimo, udhibiti wa visumbufu, matumizi ya zana bora za kilimo na huduma za ugani; ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji; ujenzi wa miundombinu ya kuhifadhi mazao ya kilimo na masoko; kufanya utafiti wa kilimo na kuzalisha teknolojia kwa mazao ya mahindi, muhogo, ngano, michikichi, ufuta, alizeti, pamba na mpunga.
14. Mheshimiwa Spika, maeneo mengine ya kipaumbele ni kuimarisha uzalishaji na upatikanaji wa mbegu bora za mazao na kusambaza kwa wakulima; kuboresha maarifa na ujuzi kwa watafiti; kuimarisha huduma za upimaji wa matabaka na ubora wa udongo kuendana na mahitaji ya mazao ya kilimo ki-ikolojia; mafunzo na usambazaji taarifa za kilimo na sayansi shirikishi; kusajili na kuandaa kanzidata ya wakulima na kuimarisha ushirika. (masuala yote ya utekelezaji wa maeneo ya kipaubele yapo kwa kina kwenye ukurasa 10-61 katika kitabu cha Hotuba ya bajeti)
15. Mheshimiwa Spika, ili kutekeleza vipaumbele hivyo, Shilingi bilioni 204.07 ziliidhinishwa na Bunge lako Tukufu. Kati ya fedha hizo, Fungu 43 – Wizara ya Kilimo iliidhinishiwa Shilingi bilioni 166.26zikiwemo Shilingi bilioni 68.14 za matumizi ya kawaida na Shilingi bilioni 98.12 za matumizi ya maendeleo; Tume ya Taifa ya Umwagiliaji - Fungu 05 iliidhinishiwa Shilingi bilioni 29.77 zikiwemo Shilingi bilioni 3.95 za matumizi ya kawaida na Shilingi bilioni 25.82fedha za maendeleo; na Tume ya Maendeleo ya Ushirika - Fungu 24 iliidhinishiwa Shilingi bilioni 8.05 zikiwa ni fedha za matumizi ya kawaida.
4.1 Kuongeza Tija katika Kilimo
Upatikanaji wa mbegu bora za mazao
16. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/2019, upatikanaji wa mbegu bora umefikia tani 49,040.66. Kati ya kiasi hicho, tani 38,507.87 zimezalishwa hapa nchini, tani 8,361.46 zimeagizwa toka nje ya nchi na tani 2,171.33 ni bakaa ya msimu wa 2017/2018. Vilevile, miche 1,507 ya miwa, vipando 121,805 vya muhogo na vikonyo 520,000 vya viazi lishe vimezalishwa. Aidha, aina mpya 13 za mbegu bora zimeidhinishwa na zitaanza kuzalishwa msimu wa 2019/2020.
Upatikanaji na udhibiti wa ubora wa Mbolea
17. Mheshimiwa Spika, hadi Machi 2019, upatikanaji na usambazaji wa mbolea nchini ulikuwa tani 492,394 ikilinganishwa na mahitaji ya tani 514,138 katika msimu wa 2018/2019. Aidha, Wizara kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imefanya ukaguzi kwa wauzaji wa mbolea 1,350 na wafanyabiashara 496 wapya wa mbolea wamesajiliwa.
Upatikanaji wa Viuatilifu na Udhibiti wa Visumbufu
18. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/2019, Wizara imenunua lita 296,000 na kilo 3,000 za viuatilifu vyenye thamani ya Shilingi bilioni tisa (9) kwa ajili ya kukabiliana na milipuko ya visumbufu vya mazao. Hadi kufikia Machi 2019, ndege waharibifu wa nafaka walidhibitiwa katika skimu za umwagiliaji za Kahe, Lekitatu na Misenyi kwa mazao ya mpunga na mtama. Aidha, lita 119,000 kwa ajili ya kudhibiti Viwavijeshi Vamizi zimesambazwa katika Kanda ya Ziwa, Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Kati, Kanda ya Magharibi, Kanda ya Kaskazini na Kanda ya Mashariki na kutoa mafunzo kwa maafisa ugani na wakulima 350.
Zana za Kilimo
19. Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonesha kwamba wastani wa kitaifa wa matumizi ya zana bora za kilimo umeongezeka hadi kufikia asilimia 20 kwa matrekta na asilimia 27 kwa wanyama kazi ikilinganishwa na asilimia 14 ya matrekta na asilimia 24 ya wanyama kazi mwaka 2013. Kutokana na ongezeko hilo, matumizi ya jembe la mkono yamepungua na kufikia asilimia 53 kwa mwaka 2018 ikilinganishwa na asilimia 62 kwa mwaka 2013. Aidha, kupitia Mfuko wa Taifa wa Pembejeo za Kilimo (AGITF) Wizara imendelea kutoa mikopo ya pembejeo na zana za kilimo. Katika kipindi cha Julai 2018 hadi Machi 2019, mikopo 33 yenye thamani ya Shilingi bilioni 1.50imetolewa.
4.2 Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Umwagiliaji
20. Mheshimiwa Spika, Tume ya Taifa ya Maendeleo ya Umwagiliaji imeendelea kusimamia utekelezaji wa Mradi wa Skimu za Umwagiliaji za Wakulima Wadogo unaofadhiliwa na Serikali ya Japan. Mradi umekarabati skimu za umwagiliaji 129 katika Halmashauri 68 nchini pamoja na ununuzi wa mitambo ya ujenzi.
4.3 Utafiti wa Kilimo na Uhaulishaji wa Teknolojia
21. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/2019, Wizara kupitia TARI imegundua mbegu bora mpya aina nne (4) za mahindi. Mbegu hizo zina uwezo wa kutoa mavuno kwa wastani wa tani 5.8 kwa hekta kwenye mashamba ya wakulima katika ukanda wa chini na kati, zinahimili ukame na zina ukinzani wa magonjwa ya majani ya mahindi na michirizi na ukungu. Vilevile, kwa kushirikiana na kampuni binafsi, TARI imezalisha aina sita (6) ya miche ya mbegu bora ya migomba na kugundua aina 62 za mbegu za mazao ya mikunde.
4.4 Maendeleo ya Mazao
22. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu utekelezaji wa mikakati ya maendeleo ya mazao mbalimbali kwa kuimarisha huduma za utafiti, upatikanaji na utumiaji wa pembejeo na zana za kilimo, udhibiti wa visumbufu vya mazao, huduma za ugani, uongezaji wa thamani na upatikanaji wa masoko. Aidha, Wizara imeandaa mkakati wa miaka minne (2018/2019 – 2021/2022) wa kuendeleza zao la michikichi.
Mazao Makuu ya Asili ya Biashara
23. Mheshimiwa Spika, uzalishaji wa mazao makuu ya biashara uliongezeka kutoka tani 901,641 msimu wa 2016/2017 hadi tani 967,184 msimu wa 2017/2018 ikiwa ni ongezeko la asilimia 7.2. Katika msimu wa 2018/2019, Wizara ililenga kuongeza uzalishaji wa mazao ya biashara hadi kufikia tani 1,356,368 na hadi kufikia Machi 2019, tani 667,631.77 sawa na asilimia 49.2 ya lengo zilikuwa zimezalishwa na uzalishaji unaendelea.
Mazao ya Bustani
24. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/2018, uzalishaji wa mazao ya bustani ulikuwa tani milioni 5.33 na matarajio ya uzalishaji kwa mwaka 2018/2019 ni tani milioni 5.96. Hadi Machi 2019, uzalishaji umefikia tani milioni 4.36 sawa na asilimia 73.17 ya lengo na msimu wa uzalishaji unaendelea.
4.5 Ujenzi wa Miundombinu ya Kuhifadhi Mazao ya Kilimo na Masoko
Miundombinu ya Kuhifadhi Mazao ya Kilimo
25. Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) inaendelea kutekeleza Mradi wa Kuongeza Uwezo wa Kuhifadhi Nafaka. Hadi kufikia mwezi Machi 2019, asilimia 83 ya vifaa vilikuwa vimeingizwa nchini kwa ajili ya ujenzi wa ghala katika vituo vya Makambako, Mbozi, Songea, Shinyanga na Dodoma.
Masoko ya Mazao ya Kilimo
26. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/2019, Wizara imeanzisha kitengo cha masoko ya mazao ya kilimo ambacho kinahusika na kutafuta masoko ndani na nje ya nchi. Katika kutekeleza jukumu hilo, Wizara imeingia makubaliano ya Itifaki ya Usafi baina ya Tanzania na Serikali ya China kuwezesha kuuza muhogo nchini China ambapo hadi mwezi Machi 2019, kampuni tano zimesajiliwa kwa ajili ya kuuza zao hilo nchini China.
Hifadhi na Usalama wa Chakula
27. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/2019, NFRA imenunua tani 46,236.035 za mahindi kwa ajili hifadhi na imeliuzia Shirika la Mpango wa Chakula Duniani tani 36,000 za mahindi zenye thamani ya Shilingi bilioni 21. Aidha, Wizara imeanza kutekeleza Mradi wa Kudhibiti Sumukuvu katika mazao unaolenga kudhibiti tatizo la sumukuvu katika mazao ya mahindi na karanga.
4.6 Huduma za Ushauri Kuhusu Utafiti, Mafunzo na Usambazaji Taarifa za Kilimo na Sayansi Shirikishi
Huduma za Ugani
28. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/2019, Wizara imeandaa rasimu ya Mwongozo wa Utoaji na usimamizi wa huduma za ugani utakaotumiwa na Sekta ya Umma na Binafsi. Aidha, elimu kuhusu kanuni bora za uzalishaji wa mazao, kuongeza thamani mazao ya kilimo, upatikanaji wa masoko, mitaji kwa ajili ya kuwekeza kwenye kilimo, pembejeo na zana bora za kilimo imetolewa kupitia maonesho na vyombo vya habari.
Vyuo na Vituo vya Mafunzo ya Kilimo
29. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/2019, Wizara kupitia Vyuo vyake vya Kilimo imedahili na kufundisha wanafunzi 2,389 ambapo wanafunzi 2,051 wamefadhiliwa na Serikali na 338 wanajilipia wenyewe. Kati ya wanafunzi waliodahiliwa, wanafunzi 1,537 ni ngazi ya Astashahada na 852 ni ngazi ya Stashahada. Jumla ya wanafunzi 1,026 wakiwemo 263 wa Stashahada na 763 wa Astashahada watahitimu masomo yao mwezi Juni, 2019.
4.7 Kuimarisha Ushirika
30. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/2019, Tume ya Maendeleo ya Ushirika kupitia Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) limefanya ukaguzi wa nje kwa vyama vya ushirika 2,297. Kati ya Vyama vilivyokaguliwa, asilimia 4.6 vilipata hati inayoridhisha, asilimia 64.6 vilipata hati yenye shaka, asilimia 21.6 vilipata hati isiyoridhisha na asilimia 9.2 vilipata hati mbaya. Hali hiyo ya Vyama vya Ushirika siyo nzuri na hatuwezi kuifumbia macho. Natoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge katika maeneo yetu tuendelee kushirikiana na Halmashauri zetu kuvisaidia vyama hivi ambavyo ni mkombozi wa mkulima.
4.8 Usajili wa Wakulima
31. Mheshimiwa Spika, Wizara imeanza usajili wakulima wote kwa mazao ambayo yanasimamiwa na Bodi. Mazao hayo ni, kahawa, korosho, miwa, pamba, chai, mkonge, tumbaku na pareto. Hadi kufikia mwezi Machi 2019, wakulima 1,464,827 wametambuliwa na kusajiliwa katika maeneo mbalimbali nchini.
4.9 Masuala Mtambuka
32. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/2019, Wizara imeendelea kuzingatia masuala mtambuka katika kutekeleza majukumu yake. Masuala hayo ni pamoja na ushiriki wa vijana katika kilimo, lishe, jinsia, hifadhi ya mazingira na VVU na UKIMWI.
5.0 MPANGO NA MAENEO YA KIPAUMBELE KWA MWAKA 2019/2020
5.1 Kuongeza Tija katika Kilimo
Upatikanaji wa mbegu bora za mazao
33. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Serikali kwa kushirikiana na Sekta Binafsi, imejipanga kuzalisha jumla ya tani 53,608.2 za mbegu mbalimbali. Wazalishaji hao ni pamoja na ASA, Vituo vya Utafiti, Magereza na Sekta binafsi. Vilevile, ASA itazalisha vipando bora vya mihogo pingili 7,000,000 na miche bora ya matunda 20,000. Ili kufikia malengo hayo, miundombinu ya umwagiliaji itaboreshwa katika mashamba yanayomilikiwa na ASA na eneo la uzalishaji wa mbegu litaongezwa hadi kufikia hekta 811 katika mashamba mbalimbali.
Upatikanaji na udhibiti wa ubora wa Mbolea
34. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara itasimamia uagizaji na usambazaji wa tani 625,000 za mbolea zinazokadiriwa kutumika nchini. Aidha, Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) itaongeza mauzo ya mbolea kutoka tani 10,000 hadi tani 100,000. Vilevile, ghala moja (1) lenye uwezo wa kuhifadhi tani 20,000 za mbolea litakarabatiwa katika wilaya ya Tabora pamoja na kuanza ujenzi wa kiwanda cha kuchanganya mbolea kwa uwiano (blending plant) katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Upatikanaji wa Viuatilifu na Udhibiti wa Visumbufu
35. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara itanunua na kusambaza lita 300,000 na kilo 3,000 za viuatilifu kwa ajili ya kukabiliana na milipuko ya visumbufu vya mazao. Aidha, Wizara itaendelea kuimarisha kituo cha kudhibiti milipuko cha Kilimo Anga (Arusha) ili kutoa huduma bora. Vilevile, Wizara itaendelea kuvijengea uwezo na kukarabati vituo 10 kati ya 36 vya ukaguzi wa mazao mipakani.
Zana za Kilimo
36. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara itaanzisha kituo kimoja (1) cha zana za kilimo kwa ajili ya kutoa huduma za kiufundi na mafunzo kwa watoa huduma binafsi wamiliki na watumiaji wa zana za kilimo kwa lengo la kusogeza huduma karibu na wakulima katika Kanda ya Ziwa. Vilevile, Wizara kupitia AGITF, imepanga kutoa mikopo 250 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 4.12.
5.2 Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Umwagiliaji
37. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji itafanya tathmini ya miradi ya umwagiliaji ambayo ujenzi wake haujakamilika ili miradi hiyo iweze kukamilishwa kwa awamu.
Aidha, kupitia Mradi wa Kuendeleza Skimu za Wamwagiliaji Wadogo, Wizara itakamilisha ujenzi wa skimu 16 za umwagiliaji katika maeneo mbalimbali.
5.3 Utafiti wa Kilimo na Uhaulishaji wa Teknolojia
38. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara kupitia TARI imepanga kutafiti, kugundua na kusambaza aina 15 za mbegu bora za mazao ya nafaka, mizizi, mbegu za mafuta, mikunde, migomba na mazao ya bustani. Vilevile, Wizara itasafisha aina tisa (9) za mbegu ya mpunga na kuzalisha tani 10 za mbegu za awali katika Kituo cha Utafiti cha KATRINI. Aidha, kupitia kituo cha TARI Naliendele, Serikali itajenga kinu cha kubangua korosho chenye uwezo wa kubangua tani 1,800 kwa mwaka na kusindika tani 1,000 za mvinyo na sharubati (juice).
5.4 Maendeleo ya Mazao
39. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara imepanga kuongeza uzalishaji wa mazao ya kipaumbele kwa kuendelea kuratibu utekelezaji wa mikakati ya maendeleo ya mazao hayo ikiwemo kuimarisha utafiti, upatikanaji na utumiaji wa pembejeo na zana za kilimo, udhibiti wa visumbufu, huduma za ugani, kuongeza maeneo ya uzalishaji, uongezaji wa thamani na upatikanaji wa masoko.
Zao la Korosho
40. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara kupitia Bodi ya Korosho itaendelea kutekeleza programu ya kuzalisha miche bora milioni 10 ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo.
Aidha, Bodi kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango itahakiki na kulipa vikundi vya wazalisha miche ya mikorosho kwa msimu wa 2017/2018 ambao hawajalipwa katika mikoa saba (7). Vilevile, Wizara itaratibu upatikanaji na usambazaji wa tani 30,000 na lita 500,000 za salfa kwa ajili ya kudhibiti visumbufu vya zao la korosho.
Zao la Miwa na Uzalishaji wa Sukari
41. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara kupitia Bodi ya Sukari itaratibu uzalishaji wa tani 403,786 za sukari kwa kuongeza eneo la uzalishaji wa kilimo cha miwa kutoka hekta 52,000 hadi hekta 97,000. Wizara, kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) itawezesha upatikanaji wa ardhi ya uwekezaji wa miradi mipya ya sukari katika Wilaya za Kasulu, Kibondo, Rufiji, Geita, Kilombero, Karagwe, Pangani, Bagamoyo na Morogoro.
Zao la Kahawa
42. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara kupitia Bodi ya kahawa itaongeza uzalishaji wa kahawa kutoka tani 65,000 hadi tani 80,000. Aidha Bodi imepanga kuzalisha na kusambaza miche milioni 10 ya kahawa katika Wilaya 42.
Zao la Mkonge
43. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara kupitia Bodi ya Mkonge imepanga kuongeza uzalishaji wa mkonge kutoka tani 38,506 hadi tani 113,506 kwa kuongeza eneo la uzalishaji kutoka hekta 42,426.11 hadi 114,915.08, kusimamia uendeshaji wa mfumo wa kilimo cha wakulima wadogo cha mkataba na kuimarisha vyama vya ushirika na masoko ya mkonge.
Zao la Pamba
44. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara kupitia Bodi ya Pamba imepanga kuongeza uzalishaji wa pamba kutoka tani 222,000 hadi tani 700,000 na tija kutoka tani 300 hadi tani 600 kwa ekari. Aidha, upatikanaji wa mbegu za pamba utaongezeka kutoka tani 22,000 hadi 40,000 na upatikanaji wa viuatilifu utaongezeka kutoka lita milioni 7 hadi milioni 10.
Zao la Tumbaku
45. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara kupitia Bodi ya Tumbaku imepanga kuongeza uzalishaji kutoka tani 55,000 hadi tani 60,000; kuimarisha vituo 1,972 vya kufungia na kuchambulia tumbaku; itaimarisha mfumo wa upatikanaji wa pembejeo za zao la tumbaku kwa kuwaunganisha watoa huduma wa pembejeo na Vyama vya Ushirika ili ziwafikie kwa wakati.
Zao la Chai
46. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara kupitia Bodi ya Chai imepanga kuongeza uzalishaji wa chai kavu kutoka tani 34,000 hadi tani 40,000 ambazo ni sawa na tani 182,000 za majani mabichi ya chai. Aidha, Wizara kwa kushirikiana na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (PSSSF) itafufua kiwanda cha chai cha Mponde ili kuimarisha upatikanaji wa soko la majani mabichi ya chai kwa wakulima na kuongeza ajira.
5.5 Miundombinu ya Hifadhi na Uongezaji Thamani Mazao ya Kilimo
47. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara kupitia NFRA itakamilisha awamu ya kwanza ya Mradi wa Kuongeza Uwezo wa Kuhifadhi ambapo ujenzi wa maghala matano (5) yenye uwezo wa kuhifadhi tani 60,000 na vihenge nane (8) vyenye uwezo wa kuhifadhi tani 190,000 za nafaka utakamilika na hivyo kuongeza uwezo wake wa kuhifadhi nafaka kutoka tani 251,000 hadi tani 501,000.
5.6 Vituo vya Utafiti huduma za Ugani na Mafunzo
Kuimarisha Vituo vya Utafiti
48. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara itakarabati ofisi na kuvipatia vifaa muhimu vituo vya utafiti vya Ukiliguru, Ilonga na Tumbi. Aidha, miundombinu ya umwagiliaji ya vituo vya utafiti vya Ilonga, Naliendele, Ukiliguru na miundombinu ya uhifadhi wa mbegu katika vituo vya Uyole, Ilonga na Seliani itaboreshwa.
Huduma za Ugani
49. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara kwa kushirikiana na OR-TAMISEMI na Sekta binafsi itakamilisha Mwongozo wa Utoaji na Usimamizi wa Huduma za Ugani Kilimo ili kuendana na mahitaji ya sasa ya utoaji wa huduma za ugani nchini.
Vyuo na Vituo vya Mafunzo ya Kilimo
50. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara itadahili wanafunzi 2,500 ngazi ya Astashahada na Stashahada kwa ufadhili wa Serikali. Vilevile, itakarabati miundombinu ikiwa ni pamoja na madarasa sita (6), ofisi 12, mabweni 12, maktaba sita (6) na mabwalo ya chakula sita (6) katika vyuo vya mafunzo ya kilimo vya Mtwara, Igurusi, HORTI Tengeru, Tumbi, Mlingano na Maruku.
5.7 Kuimarisha Ushirika
51. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Tume ya Maendeleo ya Ushirika itaimarisha udhibiti na usimamizi wa vyama vya ushirika; itahamasisha wanachama wa Vyama vya Ushirika vya Mazao kuanzisha SACCOS 1,500 kwenye maeneo yao; na itahuisha Sera ya Maendeleo ya Ushirika ya mwaka 2002 na kuipitia upya sheria za ushirika.
5.8 Uratibu, Takwimu, Ufuatiliaji na Tathmini
52. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Viwanda na Biashara, Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Zanzibar itafanya Sensa ya kilimo.
5.9 Masuala Mtambuka
53. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara itaendelea kuzingatia masuala mtambuka yakiwemo ushiriki wa vijana katika kilimo, lishe, jinsia, VVU na UKIMWI na mazingira katika utekelezaji wa majukumu yake.
5.10 Maeneo Maalum ya Maboresho katika Kilimo
54. Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie maeneo machache ya kimkakati ambayo kama Wizara tumeona ni muhimu kuyafanyia maboresho ili kuimarisha usimamizi wa kilimo na kuwapatia wakulima huduma kwa urahisi zaidi. Maeneo hayo ni kama ifuatavyo:
Mapitio ya Sera na Sheria
55. Mheshimiwa Spika, Wizara imeanza na itaendelea kuipitia Sera ya Taifa ya Kilimo ya mwaka 2013 na sheria mbalimbali kwa lengo la kubaini maeneo ambayo yatapaswa kuhuishwa ili kwenda na hali halisi ya sasa na mwelekeo wa Serikali wa kubadili kilimo chetu kuwa kilimo cha kibiashara. Mtazamo wa Wizara ni kuwa na Sheria moja itakayosimamia rasilimaliwatu, matumizi bora ya pembejeo, ardhi ya kilimo na maeneo mengine muhimu.
Bima ya Mazao
56. Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na wadau imeanza mchakato wa kuanzisha Bima ya Mazao hapa nchini ili kumwezesha mkulima kulipwa fidia pale anapopata hasara. Maandalizi yanaendelea kufanyika ili katika mwaka 2019/2020 tuwe angalau na aina mbili za mifumo ya Bima ya mazao inayoweza kutumika hapa nchini. Hata hivyo, ili utaratibu huu uwezekane, kutahitajika takwimu sahihi za hali ya hewa pamoja na uzingatiaji wa kanuni bora za Kilimo.
Usajili wa wakulima
57. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara itaimarisha kanzidata ya wakulima na kuendelea na usajili wa wakulima wa mazao mchanganyiko kwa kushirikiana kwa karibu sana na Vyama vya Ushirika na Taasisi nyingine kilele za wakulima kama vile Tanganyika Farmers Association (TFA). Ninawaomba Waheshimiwa Wabunge tusaidiane kuhamasisha wakulima katika maeneo yetu ili watakapofikiwa na zoezi la uandikishaji watoe ushirikiano na waelewe kwamba zoezi hili ni la kuwasaidia kupata huduma bora za Kilimo.
Masoko ya Mazao ya Kilimo
58. Mheshimiwa Spika, Wizara imeamua kuimarisha utafutaji wa masoko ya mazao ya kilimo ndani na nje ya nchi. Katika mwaka 2019/2020, Wizara itakiimarisha kitengo cha masoko kwa kukijengea uwezo wa kufanya uchambuzi na utafutaji wa masoko ndani na nje ya nchi.
Aidha, elimu itaendelea kutolewa kwa wakulima ili wazalishe kulingana na mahitaji ya soko. Vilevile, tutaendelea kufanya kazi kwa karibu na taasisi nyingine zinazohusika na masoko nchini ikiwemo TANTRADE na Soko la Bidhaa (TMX).
Mfumo wa upatikanaji wa Pembejeo za Kilimo
59. Mheshimiwa Spika, Wizara imeanza zoezi la kupitia kwa kina mifumo iliyopo ya uzalishaji, uagizaji na usambazaji wa mbegu, mbolea na viuatilifu. Mifumo iliyopo kwa sasa inatofautiana kwani kuna baadhi ya Bodi za Mazao zinazojihusisha na uagizaji na usambazaji wa pembejeo, wakati mwingine Vyama vya Ushirika vinaagiza na kusambaza pembejeo kwa wanachama wao, wakulima pia hununua pembejeo moja kwa moja kutoka kwa wafanyabiashara na pia mbolea kwa sasa inaagizwa kwa mfumo wa pamoja (Bulk Procurement).
60. Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa pembejeo za kilimo na tofuati ya mifumo hiyo, tumeamua kuipitia yote ili kuona mfumo bora unaoweza kutumika kuhakikisha pembejeo zenye ubora zinapatikana na kusambazwa kwa wakulima kwa wakati. Malengo yetu ni kukamilisha mapitio hayo na kupata majawabu ya mfumo bora ifikapo Juni 2019, ili mwaka 2019/2020 tuwe na mfumo madhubuti utakaokuwa na tija kwetu sote. Nina uhakika kwamba, mfumo mzuri wa upatikanaji na usambazaji wa pembejeo utawezesha uwepo wa pembejeo bora kwa bei nafuu na hivyo kuongeza matumizi kwa wakulima wetu.
61. Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina ya hotuba yangu hususan mpango na maeneo ya kipaumbele kwa mwaka 2019/2020 yanapatikana ukurasa wa 61 hadi 91 katika kitabu cha hotuba cha Wizara ya Kilimo kwa mwaka 2019/2020 kilichowasilishwa Bungeni.
6.0 SHUKRANI
62. Mheshimiwa Spika, kabla sijamaliza hotuba yangu naomba nitoe shukrani za dhati kwa watu, taasisi, makundi na wadau mbalimbali ambao tunashirikiana kuendeleza kilimo. Kwanza, nawashukuru sana, Naibu Mawaziri wa Kilimo, Mhe. Omary Tebweta Mgumba (Mb.) na Mhe. Innocent Lugha Bashungwa (Mb.) kwa ushirikiano wanaonipatia katika kutekeleza majukumu yangu. Napenda pia, kuwashukuru Katibu Mkuu, Mhandisi Mathew John Mtigumwe; Naibu Katibu Mkuu, Prof. Siza D. Tumbo; Wakurugenzi wa Idara na Wakuu wa Vitengo; Taasisi na Asasi zilizo chini ya Wizara; watumishi wote wa Wizara; na wadau wa Sekta ya Kilimo kwa juhudi, ushirikiano na ushauri uliowezesha kutekelezwa kwa majukumu ya Wizara kwa mwaka 2018/2019 pamoja na kuandaa Hotuba hii. Ni matarajio yangu kwamba, nitaendelea kupata ushirikiano wao katika mwaka 2019/2020.
63. Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kuzishukuru Nchi na Mashirika mbalimbali ya Kimataifa ambayo yamesaidia Wizara katika juhudi za kuendeleza kilimo. Nachukua fursa hii kutaja baadhi yao kama ifuatavyo: Serikali za Japan, Marekani, Uingereza, Ireland, Malaysia, China, Indonesia, Korea ya Kusini, India, Misri, Israel, Ubelgiji, Ujerumani, Finland, Norway, Brazil, Uholanzi, Vietnam, Canada na Poland. Ninayashukuru pia Mashirika na Taasisi za Kimataifa zifuatazo: Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika, AU, IFAD, DFID, UNDP, FAO, JICA, EU, UNICEF, WFP, CIMMYT, ICRISAT, ASARECA, USAID, KOICA, ICRAF, IITA, IRRI, ILRI na CABI. Nyingine ni CFC, AVRDC, AGRA, CIP, CIAT/PABRA, UNEP, WARDA, Shirika la Kudhibiti Nzige wa Jangwani na HELVETAS. Wadau wengine ni Shirika la Kudhibiti Nzige Wekundu, Bill and Melinda Gates Foundation, Gatsby Trust, Rockfeller Foundation, Aga Khan Foundation, Unilever na Asasi zisizo za kiserikali nyingi ambazo hatuwezi kuzitaja zote hapa.
64. Mheshimiwa Spika, natoa shukrani za pekee kwa wananchi wa Jimbo langu la Vwawa kwa ushirikiano wanaoendelea kunipa katika kipindi chote cha kuwawakilisha hapa Bungeni. Aidha, napenda kuwahimiza kufanya kazi kwa bidii ili kuleta maendeleo ya jimbo letu na Taifa kwa ujumla. Kwa umuhimu wa kipekee ninatoa shukrani za dhati, kwa wakulima wa nchi hii kwa kazi kubwa wanayofanya katika uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.
7.0 MAOMBI YA FEDHA MWAKA 2019/2020
65. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara inaomba idhini ya kukusanya maduhuli ya Shilingi 3,472,515,000yatokanayo na vyanzo mbalimbali vya mapato.
66. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara ya Kilimo inaomba kutumia jumla ya Shilingi 253,856,943,970 kupitia Fungu 43, Fungu 05 na Fungu 24 kama ifuatavyo;
FUNGU 43 – Wizara ya Kilimo
67. Mheshimiwa Spika, jumla ya Shilingi 208,044,783,140zinaombwa. Kati ya fedha hizo, Shilingi 143,577,036,140 ni kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ambapo Shilingi 82,000,000,000ni fedha za ndani na Shilingi 61,577,036,140 ni fedha za nje. Aidha, Shilingi 64,467,747,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida ambapoShilingi 13,214,159,060 ni kwa ajili ya mishahara ya Wizara, Shilingi29,621,801,490 ni kwa ajili ya mishahara ya Bodi na Taasisi, Shilingi11,453,309,490 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo kwa Wizara naShilingi 10,178,476,510 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo kwa Bodi na Taasisi.
FUNGU 05 – Tume ya Umwagiliaji
68. Mheshimiwa Spika, jumla ya Shilingi 37,485,090,830zinaombwa. Kati ya fedha hizo, Shilingi 32,501,462,613 ni kwa ajili ya kutekeleza Miradi ya Maendeleo ambapo Shilingi 3,000,000,000 ni fedha za ndani na Shilingi 29,501,462,613 ni fedha za nje.
Aidha, Shilingi 4,983,628,217 zinaombwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ambapo Shilingi 4,098,444,217 ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa Tume na Shilingi 885,184,000 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo.
FUNGU 24 – TUME YA USHIRIKA
69. Mheshimiwa Spika, jumla ya Shilingi 8,327,070,000 zinaombwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ambapo Shilingi6,127,370,000 kwa ajili ya mishahara na Shilingi 2,199,700,000kwa ajili ya matumizi mengineyo.
Maelezo ya sehemu ya maombi ya fedha mwaka 2019/2020 kwa fungu 43, 65 na fungu 24 yanapatikana ukurasa wa 93 hadi 95 katika kitabu cha hotuba ya bajeti ya Wizara ya Kilimo.
HITIMISHO
70. Mheshimiwa Spika, Pamoja na hotuba hii, vipo viambatisho vinavyotoa ufafanuzi wa baadhi ya maeneo. Hotuba hii pia inapatikana katika tovuti ya Wizara ya Kilimo, www.kilimo.go.tz. Ninaomba kuhitimisha kwa kukushukuru wewe binafsi na Waheshimiwa Wabunge wote kwa kunisikiliza.
71. Mheshimiwa Spika, NAOMBA KUTOA HOJA
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Social Plugin