Waziri wa mambo ya nje wa Iran Mohammed Javad Zarif amesema kile alichokiita ''kejeli za maangamizi'' za rais wa Marekani Donald Trump haziwezi kuimaliza Iran.
Kupitia mtandao wa Twitter, Zarif amesema Iran imesimama imara kwa maelfu ya miaka, wakati maadui wake wote wakiwa wametoweka.
Haya Zarif anayasema wakati mvutano ukizidi kushamiri baina ya nchi yake na Marekani, na onyo la Trump kwamba ikiwa Iran haitaacha kuitishia Marekani, basi mwisho rasmi wa Iran utakuwa umewadia.
Mahusiano baina ya nchi hizo mbili yalizidi kuzorota mwaka jana baada ya Rais Trump kuiondoa Marekani katika makubaliano kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, yaliyosainiwa mwaka 2015 kati ya taifa hilo la Kiislamu na nchi zenye nguvu duniani.
Mvutano huo ulichukuwa sura mpya mwezi huu pale Marekani ilipopeleka katika eneo la Ghuba manowari na ndege za kivita chapa B-52 kujibu ilichokitaja kuwa kitisho kutoka Iran ambacho haikukifafanua.
Social Plugin