Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov amelaani vikali uungaji mkono wa Marekani kwa kinara wa upinzani nchini Venezuela Juan Guaido ambaye alikuwa amedai amepata uungaji mkono wa jeshi katika jaribio lililofeli la kumpindua Rais Nicolas Maduro.
Lavrov aliyasema hayo jana Jumatano wakati akizungumza kwa simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo ambapo amemfahamisha bayana kuwa, uingiliaji wa Marekani katika masuala ya ndani ya Venezeula ni ukiukwaji wa wazi wa sheria za kimataifa.
Lavrov aidha amekosoa vitisho vya wakuu wa Marekani hasa Rais Donald Trump kuhusu kutumia nguvu za kijeshi dhidi ya Rais Maduro na kusema, utekelezwaji wa hatua kama hizo utakuwa na matokeo mabaya.
Jumanne April 30, Caracas, mji mkuu wa Venezuela ulipitia siku ngumu na iliyojaa mitihani.
Kwa mara nyingine Marekani na watu wanaodaiwa kuwa vibaraka wake wa ndani wanaoongozwa na Juan Guaido aliyejitangaza kuwa Rais na ambao wanaendesha vurugu na upinzani dhidi ya serikali ya nchi hiyo walifanya jaribio la mapinduzi dhidi ya serikali ya mrengo wa kushoto inayoongozwa na Nicolas Maduro, kwa kushirikiana na baadhi ya wanajeshi, lakini kwa mara nyingine tena Marekani ikawa imeshindwa katika jaribio lake hilo la mapinduzi nchini Venezuela.
Huku akisisitiza kuwa jaribio la mapinduzi ya kijeshi dhidi ya serikali halali ya nchi hiyo limefeli, Jorge Arreaza, Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela amesema kwamba licha ya juhudi zote zinazofanywa na wapinzani na serikali ya Washington kwa ajili ya kuupindua mfumo wa kisiasa wa Venezuela, lakini bado Rais Nicolas Maduro anaidhibiti nchi kwa uungaji mkono wa wananchi na jeshi.
Akizungumza juzi akiwa katika uwanja wa ndege wa kikosi cha anga cha La Carlota katika viunga vya mji wa Caracas, Juan Guaido alidai kuwa jeshi haliko tena pamoja na Nicolas Maduro na hapo akatangaza rasmi kuanza kwa operesheni aliyoitaja kuwa ni ya 'kuikomboa Venezuela.'
Licha ya matamshi hayo , wanajeshi watiifu kwa serikali halali ya Venezuela wangali wanamuunga mkono Rais Maduro pamoja na katiba ya nchi hiyo na wamefanikiwa kufelisha jaribio hilo la mapinduzi kwa ushirikiano wa wananchi.
Baada ya kushindwa mapinduzi hayo, Vladimir Padrino López, Waziri wa Ulinzi wa Venezuela amesema: 'Wanajeshi wa nchi hii wamesimama imara kulinda katiba na serikali halali ya Venezuela.'
Hali ya hivi sasa ya Venezuela na hasa kushindwa kwa mapinduzi hayo kumeamsha hasira ya viongozi wa Washington kwa kadiri kwamba mara tu baada ya kushindwa mapinduzi hayo, John Bolton, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani, alikariri misimamo ya chuki ya nchi hiyo dhidi ya Caracas na kutishia kwamba bado machaguo yote yako mezani dhidi ya Venezuela ikiwemo kuivamia kijeshi.
Maafisa wa Marekani pia wamedai kwamba uungaji mkono wa baadhi ya nchi za kigeni zikiwemo Urusi na Cuba kwa Venezuela ndio umepelekea kushindwa mapinduzi hayo.
Marekani inadai kuwa kurejesha demokrasia Venezuela, kuboresha uchumi wa nchi hiyo na kupeleka huko misaada ya kiuchumi, chakula na madawa ndiko kumeifanya itake kuiondoa madarakani serikali halali ya Maduro, katika hali ambayo viongozi wa Caracas wanasema kuwa hali mbaya ya nchi hiyo imesababishwa na siasa za vikwazo za Washington na msimamo wake wa kuongeza mashinikizo ya kisiasa na kiuchumi dhidi ya nchi hiyo.
Kwa mtazamo wa viongozi wa Venezuela, Marekani inafanya juhidi za kuhuisha nafasi yake ya zamani katika nchi za Amerika ya Latini na hasa nchini Venezuela ambayo ina utajiri mkubwa wa mafuta.
Akizungumzia suala hilo, Igor Kostyukov, Mkuu wa Idara ya Intelijensia ya Jeshi la Russia GRU, huku akiashiria kwamba kila mwaka Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani hutumia kwa uchache dola bilioni moja na nusu kwa ajili ya kuongeza ushawishi wake katika eneo la Amerika ya Latini, ameonya kwamba kuna uwezekano mkubwa wa Marekani kutumia hivi karibuni 'mapinduzi ya njano' ambayo inayatekeleza sasa huko Venezuela kwa ajili ya kuziangusha serikali za Nicaragua na Cuba.
Hali ya hivi sasa ya Venezuela ni tata mno. Viongozi wa Venezuela wakiwemo wanajeshi wametangaza kwamba wanadhibiti hali ya mambo nchini humo na kwamba jaribio la mapinduzi limeshindwa.
Kwa mara nyingine jeshi limetangaza utiifu wake kwa serikali ya Maduro na wananchi wameitikia kwa wingi mwito uliotolewa na chama cha Umoja wa Kisoshalisti kwa ajili ya kukusanyika mbele ya ikulu ya nchi hiyo.
Katika upande wa pili, Juan Guaido ambaye anaungwa mkono kwa hali na mali na utawala wa Washington amewataka wafuasi wake waingie mitaani.
Viongozi wa Washington wamekerwa sana na jinsi mambo yalivyobadilika kinyume na matarajio yao na wanafuatilia kwa karibu mno matukio ya Venezuela.
Social Plugin