Uchimbaji kaburi atakalozikwa aliyekuwa Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni za IPP, Reginald Mengi umeanza leo asubuhi Jumatatu Mei 6, 2019 nyumbani kwake Kijiji cha Nkuu Sinde Machame Mashariki, mkoani Kilimanjaro, eneo ambalo walizikwa wazazi wake na mwanae, Roodney Mengi aliyefariki mwaka 2005.
Mfanyabiashara huyo maarufu ndani na nje ya Tanzania alifariki dunia usiku wa kuamkia Alhamisi Mei 2, 2019 akiwa Dubai, Falme za Kairabu alikokuwa akipatiwa matibabu.
Mwili wa Mengi umewasili leo Jumatatu saa 9:00 alasiri katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam (JNIA), kisha utapitishwa barabara mbalimbali hadi Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo.
Kesho mwili huo utaagwa katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam, baadaye utapelekwa nyumbani kwake Kinondoni utakapolala hadi Jumatato asubuhi utakaposafirishwa kwenda Machame kwa mazishi yatakayofanyika Alhamisi hii Mei 9, 2019.
Social Plugin