Na Greyson Mwase, Chunya
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila amezindua Soko la Madini Chunya ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ya kutaka Wilaya ya Chunya kuhakikisha imekamilisha na kuzindua soko la madini ndani ya kipindi cha siku saba. Rais Magufuli alitoa agizo hilo tarehe 27 Aprili, 2019 wilayani Chunya katika mkutano wake na wachimbaji na wachenjuaji wa madini.
Uzinduzi huo ulishirikisha Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula, Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mary-Prisca Mahundi, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu kutoka Wizara ya Madini, Issa Nchasi, Mhasibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Anthony Tarimo na Kamishna Msaidizi- Uendelezaji wa Migodi kutoka Wizara ya Madini, Ali Ali.
Wengine walioshiriki katika uzinduzi huo ni pamoja na Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini kutoka Tume ya Madini, Dk. Venance Mwase, wawakilishi wa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini, viongozi wa dini pamoja na vyombo vya habari.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Profesa Msanjila alisema kuwa, tangu kuingia madarakani kwa Serikali ya Awamu ya Tano, imekuwa ikisisitiza dhamira yake ya kuhakikisha Sekta ya Madini inakua, inanufaisha watanzania pamoja na kuchangia ukuaji wa Pato la Taifa.
Akielezea mafanikio ya Serikali kupitia Wizara ya Madini kwenye usimamizi wa rasilimali za madini, Profesa Msanjila alisema kuwa, ili kuhakikisha kuwa wananchi wote wananufahika na rasilimali za madini, Serikali ilitunga Sheria ya Mamlaka ya Nchi Kuhusiana na Umiliki wa Maliasili Namba 5 ya Mwaka 2017; Sheria ya Mapitio na Majadiliano Kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba ya Maliasili za Nchi Namba 6 ya mwaka 2017 pamoja na kufanya marekebisho ya Sheria ya Madini Sura ya 123.
Aliendelea kueleza kuwa Serikali pia imefuta baadhi ya tozo ambazo zilikuwa kero kwa wafanyabiashara wa madini hususan wachimbaji wadogo na kufafanua kuwa tozo hizo kuwa ni pamoja na kodi ya ongezeko la thamani (VAT) asilimia 18 na kodi ya zuio ya asilimia tano kwa wachimbaji wadogo.
Alisema kuwa, kuwekwa kwa mazingira mazuri ya kibiashara kwenye sekta ya madini pamoja na kufuta kodi na tozo mbalimbali zinazofikia asilimia 23 kutaondoa utoroshwaji wa madini na kusaidia wachimbaji wadogo kutambuliwa kupitia uanzishwaji wa masoko ya madini.
Alieleza manufaa mengine kuwa ni pamoja na kupunguza gharama za uendeshaji wa shughuli za wachimbaji wadogo na kuongeza wigo wa mapato ya nchi.
Katika hatua nyingine, Profesa Msanjila aliwataka wachimbaji wote wadogo na wafanyabiashara wa madini kuendelea kushirikiana na mamlaka mbalimbali za Serikali katika kutekeleza majukumu yao kwa kufuata sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali inayotolewa na Serikali.
Akielezea manufaa ya soko jipya la madini Chunya, Profesa Msanjila alisema soko litaziba mianya ambayo imekuwa chanzo cha utoroshwaji wa madini, ukwepaji kodi na hivyo kusababisha biashara nzima ya madini kufanyika kiholela katika maeneo mengi ya nchi.
Aliongeza kuwa kuanzishwa kwa Soko la Madini Chunya kutawezesha na kurahisisha biashara nzima ya madini na kuwa kiungo muhimu cha kuwakutanisha wachimbaji na wafanyabiashara kwa lengo la kuuza na kununua madini.
Profesa Msanjila aliendelea kufafanua manufaa mengine ya soko kuwa ni pamoja na kuwa suluhisho la tatizo la kupunjwa na kudhulumiwa na kuondoa vitendo vya dhuluma ambavyo vimekuwa vikiwahusisha wafanyabiashara wa madini wasiokuwa waaminifu kwa baadhi ya wachimbaji wadogo.
“Soko hili litaondoa uwezekano wa wanunuzi wa madini kuibiwa na wajanja wachache wanaojifanya kuwa na madini wakati hawana, nawasihi wanunuzi wa madini kulitumia soko kikamilifu ili kuepuka udanganyifu na matapeli tu” alisema Profesa Msanjila.
Katika hatua nyingine Profesa Msanjila aliupongeza uongozi wa Wilaya ya Chunya, wafanyabiashara wa madini kwa kuhakikisha Soko la Madini Chunya limezinduliwa ndani ya muda uliopangwa.
Wakati huo huo akizungumzia hali ya uanzishwaji wa masoko ya madini nchini, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula alisema kuwa, hadi kufikia sasa masoko matano ya madini yameshafunguliwa katika mikoa ya Geita, Singida, Kahama, Arusha – Namanga na Chunya.
Aliongeza kuwa masoko mengine ya madini yanatarajiwa kufunguliwa kabla ya tarehe 05 Mei, 2019 ikiwa ni pamoja na Soko la Madini ya Dhahabu na Vito vya Thamani Ruvuma, Soko la Madini Shinyanga, Soko la Madini Dodoma na Soko la Madini Mbeya.
Profesa Kikula alitaja masoko mengine ambayo yanatarajiwa kufunguliwa hivi karibuni kuwa ni pamoja na Soko la Madini ya Bati (tin) na Soko la Madini ya Dhahabu Handeni.
Alisisitiza kuwa mikoa mingine ipo katika hatua za mwisho kukamilisha vigezo mbalimbali vikiwemo vya kiusalama na miundombinu.
Social Plugin