Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RIDHIWANI KIKWETE AANZISHA UJENZI WA SHULE YA MSINGI


Na Shushu Joel, Chalinze. 
Mbunge wa jimbo la chalinze wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani Ridhiwani Kikwete amekuwa wa kwanza kuchangia mifuko 20 ya saruji kwa ajili ya uanzishwaji wa ujenzi wa shule ya msingi katika kitongoji cha choza,Kata Ubena Zomozi ili kusaidia watoto wa maeneo hayo.

Akizungumza na viongozi mbalimbali wa kata,vijiji na vitongoji wa kata hiyo alisema kuwa amefanya  maamuzi hayo ya kuanzisha ujenzi wa shule hiyo kutokana na changamoto zinazowakabili wazazi/walezi na wanafunzi kwa kutembea umbali mrefu kwa ajili ya kupata elimu ya shule ya msingi huku wazazi kwa ajili ya masuala ya kimaendeleo.

Alisema kuongezeka kwa watu katika hilo eneo la Choza kimepelekea kuhitajika kwa haraka kwa huduma za kijamii ili kuendana na mahitaji ya wakazi wa eneo hilo.

"Saruji niliyotoa ni uanzilishaji wa ujenzi wa shule hiyo lakini si kwamba ndio mwisho wa utoaji wangu wa mahitaji katika ujenzi huo bali ni kama kiongozi wa mfano ili hata wananchi wanapoambiwa wachangie  wasisite" ,alisema Ridhiwani Kikwete 

Aidha aliongeza kuwa wananchi ndiyo nguzo ya maendeleo hivyo wanapoamua jambo lolote lile la kimaendeleo ni lazima lifanyike kutokana na umoja, nguvu na mshikamano wao katika ufanikishaji wa maendeleo katika eneo husika.

Pia mara baada ya kutoa mifuko hiyo ya saruji Ridhiwani aliwataka viongozi wa eneo hilo kutafuta eneo jingine  kubwa lenye kufaa ujenzi wa zahanati ili pia Choza pajengwe zahanati.

Pia amewataka wananchi wa Choza kujitokeza kwa wingi  katika kuhamasishana  juu ya maendeleo kwani serikali inatambua  makusudi yao.

Kwa upande wake diwani wa kata hiyo ya Ubena  Zomozi Nicholaus  Muyuwa amempongeza Mbunge huyo kwa uanzilishi wake wa kutoa saruji kwa lengo la ujenzi wa shule katika eneo hilo ili kuwaondolea changamoto watoto wa maeneo hayo.

Aidha amemhakikishia Ridhiwani kuwa saruji hiyo itatumika kama ilivyokusudiwa kufanyika kwani hata wao walikuwa wakilifikiria tu lakini Mbunge huyo kafanya kweli. 

Naye Cosmos Alphonce ni Mwenyekiti wa kijiji cha Kaloleni ameshukuru kwa mchango uliotolewa na mbunge na kumtaka aendelee na moyo huo wa kujitolea kwa wananchi wake.

Aliongeza kuwa kujengwa kwa shule katika eneo hilo kutaondoa changamoto ya watoto wa eneo hilo kutembea kilometa  nyingi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com