Shahidi wa tatu, katika kesi ya uchochezi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na viongozi wenzake nane, Koplo Rahim amedai baadhi ya waandamanaji walivaa mzula hawakuonekana nyuso zao.
Amedai walikuwa wanarusha mawe na jiwe moja lilimpiga shingoni akapoteza fahamu na hakujua mahali ambako silaha yake aina ya SMG ilipo.
Koplo Rahim amesema hayo leo asubuhi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akiongozwa na Wakili wa Serikali, Simon Wankyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thoma Simba.
Amedai wanachama wa Chadema wakiongozwa na viongozi wao waliandamana kutoka viwanja vya buibui kuelekea kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni wakiwa na mawe, chupa za maji na baadhi walivaa mzula hawakuonekana nyuso zao.
Waandamamaji walizuia kuandamana lakini walikaidi ndipo ilipotolewa amri ya kuwapiga mabomu ya machozi ili wasiendelee.
“Moshi wa mabomu ya machozi ulikuwa unarudishwa na upepo upande ambao tulikuwepo askari, moshi ulirudi kwetu, nilipigwa jiwe nikapoteza fahamu, nikipelekwa Polisi Kilwa Road kwa matibabu, nililazwa hapo, nilipopata fahamu nikakumbuka sina silaha, sijui nani alinipiga jiwe.
“Alikuja afande Ndelengi hospitali nikamuuliza kuhusu silaha yangu, akaniambia alichukua mwenzangu iko Oystebay, ilirudishwa ikiwa na silaha zake.
Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ya uchochezi ni Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Salum Mwalimu na Naibu katibu Mkuu bara na Mbunge wa kibamba John Mnyika, mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe Halima Mdee, Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya, Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko na katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk Vincent Mashinji na Mchungaji Peter Msigwa.
Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari mosi na 16, mwaka 2018, Dar es Salaam.
Social Plugin