Said Rashid (36), mkazi wa Mbezi Juu jijini Dar es Salaam amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni akikabiliwa na shtaka la kumbaka mwanaye mwenye umri wa miaka 13.
Akisoma hati ya mashtaka jana Jumatano Mei 29, 2019 mbele ya hakimu, Anifa Mwingira, wakili wa Serikali, Matarasa Hamisi amedai kati ya mwaka 2016 na 2019 mshtakiwa alimbaka mtoto wake huku akijua kufanya hivyo ni kosa la kisheria.
Matarasa amedai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuomba mahakama kupanga tarehe nyingine ya kutajwa.
Wakati mshtakiwa huyo akikana kufanya kitendo hicho Hakimu Mwingira alieleza kuwa dhamana ipo wazi, akimtaka kuwa na wadhamini wawili wanaotambulika kisheria watakaosaini bondi ya Sh1 milioni kila mmoja.
Hata hivyo, mshtakiwa alishindwa kutimiza masharti ya dhamana na kupelekwa rumande hadi Juni 10, 2019.
Na Pamela Chilongola, Mwananchi
Social Plugin