MADURO ALIPONGEZA JESHI LA VENEZUELA KWA KUZIMA JARIBIO LA MAPINDUZI


Rais Nicolás Maduro wa Venezuela amelipongeza jeshi la nchi hiyo kwa kuzima jaribio la mapinduzi dhidi ya serikali yake, harakati ambazo anasema zinaungwa mkono na Marekani.

Maduro amesema Marekani ndiyo iliyochochea na kufadhili kwa hali na mali ghasia zilizoshuhudiwa jana katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo ya Amerika ya Latini, lakini amesisitiza kuwa vyombo vya usalama vilifanikiwa kuzima ghasia hizo.

Amesema asilimia 80 ya askari waliotangaza jana kuliasi jeshi na kuyauga mkono maandamano ya wananchi walirubuniwa kufanya hivyo, lakini walipogundua kuwa hizo zilikuwa njama za vinara wa upinzani nchini humo Juan Guaidó na Leopoldo Lopez waliachana na njama hizo.

Vladimir Padrino López, Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo sambamba na kupongeza juhudi za Rais Maduro kwa ajili ya kuimarisha usalama na demokrasia, amesema kuwa jeshi lingali linamuunga mkono kikamilifu rais wa nchi hiyo aliyeingia madarakani kwa kura za wananchi.

Hii leo waungaji mkono wa serikali ya mrengo wa kushoto ya Caracas wanatazamiwa kufanya maandamano makubwa na kuonyesha uungaji mkono wao kwa serikali ya Maduro, mkabala wa ubeberu na njama za Washington.

Mgogoro unaoshuhudiwa hivi sasa nchini Venezuela ulishtadi mwezi Januari mwaka huu baada ya Juan Guaidó, kiongozi wa upinzani ambaye ni kibaraka wa Marekani na madola ya Magharibi, kujitangaza kuwa rais wa muda wa Venezuela, suala ambalo linakiuka katiba ya nchi hiyo.

Jana Jumanne, Guaido alitangaza kuwa ni siku ya kwanza ya duru ya mwisho ya 'harakati za ukombozi' za kumng'oa madarakani Rais Maduro.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post