Na James Magai, Mwananchi
Dar es Salaam. Mahakama Kuu Tanzania imebatilisha vifungu vya Sheria ya Uchaguzi vinavyowapa mamlaka wakurugenzi wa halmashauri za majiji, miji, wilaya na manispaa kuwa wasimamizi wa uchaguzi kwa niaba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Uamuzi huo umetolewa leo Ijumaa Mei 10, 2019 na jopo la majaji watatu wa Mahakam a Kuu, ambao waliongozwa na Jaji Atuganile Ngala. Wengine ni Dk Benhajj Masoud na Firmin Matogolo.
Kesi hiyo namba 6 ya mwaka 2018, ilifunguliwa na watetezi na wanaharakati wa haki za binadamu na demokrasia kwa kushirikiana na vyama vya siasa, vilivyowakiwakilishwa na mwanachama wa Chadema, Bob Wangwe dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Kwa mujibu wa hati ya madai ya kesi hiyo, Wangwe ambaye alikuwa mdai pekee alikuwa anapinga wakurugenzi wa halmashauri za wilaya, manispaa na au majii kuwa wasimamizi wa uchaguzi.
Pamoja na mambo mengine alikuwa akidai kuwa wakurugenzi hao ni wateule wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye kwa sasa ndiye mwenyekiti wa CCM, ambacho pia huwa kinashiriki katika uchaguzi.
Pia alikuwa anadai kuwa sheria hiyo ni kinyume cha Ibara ya 74 (14 ) ya Katiba ambayo inapiga marufuku mtu yeyote anayehusika na uchaguzi kuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa na kwamba ana haki ya kupiga kura tu.
Katika uamuzi wake leo, mahakama hiyo imekubaliana na hoja za mdai dhidi ya hoja za Serikali iliyokuwa ikitetea wakurugenzi hao kuendelea kuwa wasimamizi wa uchaguzi kwa madai kuwa suala hilo haliathiri uchaguzi kwa kuwa uteuzi wao ni kwa mujibu wa sheria.
Akisoma uamuzi huo, Jaji Ngala alisema vifungu 7(1) na 7(3) vya Sheria ya Uchaguzi ni vinakiuka Katiba kwa kuwa vinakwenda kinyume na matakwa ya kikatiba ya uhuru wa Tume ya Uchaguzi.
Kifungu cha 7(1) ndicho kinachowapa mamlaka wakurugenzi kuwa wasimamizi wa uchaguzi kwa niaba ya NEC.
Hata hivyo, akisoma uamuzi huo Jaji Ngala amesema vifungu hivyo vinakinzana na Katiba ya Nchi kwa kuwa wakurugenzi ni wateule wa Rais na hawako chini ya tume na kwamba Katiba inaelekeza Tume yan Uchaguzi iwe huru.
Jaji Ngwala amesisitiza kuwa sheria hiyo haihakikishi kuwa wakurugenzi hao watakuwa huru katika utekelezaji wa majukumu yao.
Amesema wameridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mdai kuwa wakurugenzi wengi ni wanachama wa CCM kwa kuwa kuna wakurugenzi 74 ambao orodha yao imewasilishwa mahakamani ambao ni wanachama wa chama hicho tawala.
Kifungu 7(3) kinaeleza kwamba NEC inaweza kumteua mtu yeyote kuwa msimamizi wa uchaguzi.
Mahakama hiyo imesema kuwa hata kifungu hicho hakiweki ulinzi kuhakikisha kuwa watu hao wanakuwa huru na kwamba lazima kuwe na ulinzi kwa kuhakikisha kuwa anayeteuliwa si mwanachama wa chama chochote cha siasa.
“Kwa hiyo tunatamka kwamba vifungu hivi ni kinyume cha Katiba ya nchi inayotaka kuwe na uhuru wa tume katika utekelezaji wa majukumu yake,” amesema Jaji Ngwala.
Akuzungumza baada ya uamuzi huo, Fatme Karume, ambaye alikuwa wakili wa Wangwe, amesema kwa uamuzi huo sasa hakuna wasimamizi wa uchaguzi na kwamba itabidi NEC itumie kifungu cha 7(2) cha sheria hiyo kuteua wasimamizi huru.
Karume ameleezea kufurahishwa na uamuzi wa mahakama kwa kutotoa amri kwa Serikali ya kufanya marekebisho ya sheria hiyo wala kuipa muda, akisema kwa uamuzi huo kuanzia sasa kifungu hivyo ni batili.
Amesema kwamba maana yake imevifuta moja kwa moja badala ya kuipa serika nafasi .
“Kwa hiyo nimefurahi sana, sana kwa uamuzi huu kwa sababu hatukuwa na tume huru kwa kuwa wale waliokuwa na jukumu la kuhesabu na kuhakikisha kuwa kura ziko salama hawakuwa huru,” amesema Wakili Karume.
“Kwa sababu hawako chini ya Tume bali wako chini ya Rais na chama tawala.”
Kwa upande wake, Wangwe amesema amefurahishwa na ushindi huo na kwamba si wake wala Karume pekee, bali ni wa watu wote wapenda demokrasia na hata wale wasiopenda harakati hizo.
“Hili ni fundisho kwamba katika kupigania utawala bora katika nchi, katika kupigania demokrasia katika nchi hii, ni suala la kila Mtanzania, kila mtu anangalie wapi kuna mapungufu, sheria gani ambazo ni mbovu, mahakama hizi ziko kwa ajili yetu,” amesema Wangwe.