MUME NA MKE WANUSURIKA KICHAPO KWA KUZIKA MAITI BANDIA

Mtu na mke wake huko Homa Bay nchini Kenya wamenusurika kipigo  baada ya jamaa zao kugundua walikuwa wakitaka kuzika watoto bandia.
Tukio hilo limetokea siku ya  Jumatano, Mei 8,2019

Beryl Akinyi, na mume wake Benson Onyango, 38, hatimaye walitiwa mbaroni na kupelekwa katika kituo cha Polisi cha Mbita huku polisi wakianzisha uchunguzi kuhusu kisa hicho. 

 Onyango ambaye ni seremala alitengeneza majeneza mawili na kuyapeleka uwanja mdogo wa ndege wa Kabunde alikokuwa akitarajiwa mke na ‘maiti’. 

 Ilivyoripotiwa katika The Standard, wawili hao walidai pacha wao waliaga dunia mara baada ya kuzaliwa na kuongeza kuwa Akinyi alipatwa na matatizo wakati akijifungua pacha wao. 

“Tunachunguza kisa hiki ili kupata ukweli,” alisema afisa wa polisi anayehusika na uchunguzi wa kisa hicho.

 “Tunataka kufahamu ikiwa mke alimhadaa mume wake kuhusu ujauzito wake au la. Ama ikiwa walishirikiana kufanya ukora huo tutajua tu ” aliongeza kusema. 

Wananchi walisema walifukua ‘miili’ mara baada ya kuzikwa na kugundua ni kweli haikuwa maiti bali watoto bandia waliokuwa wamefungwa katika shuka. 

Shemeji yake Akinyi, Wycliffe Ogembo, alisema alitoka nyumbani siku kadhaa na kudai alikuwa akienda kujifungua katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Homa Bay lakini aliwaarifu alishauriwa kwenda Hospitali ya Aga Khan, Kisumu.

Ogembo alisema walishuku madai ya Akinyi ambaye alikuwa amedai alijifungua mtoto wa kwanza kupitia upasuaji Homa Bay kisha kuhamishiwa Kisumu.

 “Haiwezekani yeye kuwa Homa Bay, Agha Khan na alikuwa amelazwa Hospitali Kuu ya Kenyatta,” Ogembo alisema.

 Siku kadhaa baadaye, Akinyi na Onyango walidai pacha wao waliaga dunia walipokuwa wakizaliwa na hali hiyo iliwashangaza sana na ndipo wakaanza kujiuliza maswali.

Jumanne, Mei 7,2019 mume ambaye ni fundi seremala alitengeneza majeneza mawili na kuyapeleka uwanja mdogo wa ndege wa Kabunde alikokuwa akitarajiwa kuwasili mke na ‘maiti’.

Inadaiwa walisafirisha ‘maiti’ ndani ya Toyota Probox, na walipofika nyumbani wakaamua kuzika bila ya kuwafahamisha jamaa zao. 

Haijabainika wazi ikiwa Akinyi, aliyeonekana na ujauzito alijifungua au la ingawa inashukiwa aliwauza watoto wake madai ambayo bado hayajathibitishwa.

 Kamanda wa Polisi Homa Bay, Esther Seroney, alithibitisha tukio hilo na kusema watampeleka Akinyi hospitalini kuthibitisha madai yake. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post