Makamu wa Kwanza wa Rais wa Bunge la Afrika Mheshimiwa Stephen Masele amempongeza kupitia ukurasa wake wa tweeter kiongozi wa chama cha Economic Freedom Fighters (EFF) Julius Malema kwa kupata viti vingi vya ubunge kwenye uchaguzi mkuu nchini Afrika Kusini uliofanyika Mei 8 2019.
Ukilinganisha na ushindi waliopata miaka mitano iliyopita. EFF ndio chama pekee kilichoongeza viti vingi ukilinganisha na vyama vikongwe kama ANC iliyopoteza viti 19 na Chama Cha DA Pia kimepoteza viti 6.
Malema “The Son of the Soil", kama anavyotambulika na wafuasi wa chama chake cha Economic Freedom Fighters (EFF), ameweza kuongeza viti 18 bungeni nakufikisha viti 44 ikilinganisha na viti 26 vya kipindi kilichopita.
Masele ambaye ni Mbunge wa jimbo la shinyanga Mjini na Malema ni marafiki wa karibu na wa muda mrefu tangu wakiwa viongozi wa vijana wa vyama vya CCM na ANC. Pia ni wabunge wa Bunge la Afrika ambalo Makao Makuu yako nchini Afrika kusini.
Viongozi hao vijana wameonekana jijini Johannesburg wakiwa pamoja wakipongezana.Masele ambaye yuko nchini Afrika kusini kikazi katika Bunge la Afrika.
Mheshimiwa Masele pia amempongeza kiongozi wa chama tawala ANC ,Rais Cyril Ramaphosa kwa ushindi wa chama chake. Rais Ramaphosa anatarajiwa kuchaguliwa na Bunge la Afrika kusini kuwa Rais wa nchi hiyo.
Uchaguzi mkuu wa mwaka huu umekuwa chini uangalizi wa taasisi mbalimbali za kimataifa ambapo timu ya Umoja wa Afrika ilikuwa ikiongozwa na Rais mstaafu wa Tanzania Mhe. Jakaya Kikwete.
Rais mstaafu wa Tanzania Mhe. Jakaya Kikwete (wa nne kulia) akiwa na Kiongozi wa chama cha ANC na Rais wa Afrika Kusini Mhe. Cyril Ramaphosa katika ukumbi wakati wa kutangaza rasmi matokeo ya uchaguzi mkuu wa Afrika Kusini 2019. Mhe. Kikwete ndiye Kiongozi wa timu ya uangalizi wa uchaguzi huo ya Umoja wa Afrika.
Kwa mujibu wa tume ya uchaguzi ya nchi hiyo, shughuli za kuhesabu kura katika uchaguzi huo zimekamilika kwa asilimia 100 na chama tawala nchini Afrika ya Kusini African National Congress (ANC) kimepata asilimia asilimia 57.5 ikiwa ni ushindi mdogo zaidi kwa chama hicho ambacho kimeitawala Afrika ya Kusini tangu kukomeshwa kwa utawala wa ubaguzi wa rangi miaka 25 iliyopita.
Idadi ya watu waliopiga kura nchini humo imeshuka baada ya asilimia 65 pekee ya raia kujitokeza katika uchaguzi huo.
Chama cha upinzani cha Democratic Alliance (DA) kimejipatia asilimia 20.7 ya kura huku chama cha Economic Freedom Fighters (EFF) cha Julius Malema kikijipatia asilimia 10.7 ikiwa ni mafanikio ikilinganishwa na asilimia 6.3 ya kura ilizopata chama hicho miaka mitano iliyopita.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Bunge la Afrika Mheshimiwa Stephen Masele akikumbatiana na Kiongozi wa chama cha Economic Freedom Fighters (EFF) cha Julius Malema Mei 11,2019
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Bunge la Afrika Mheshimiwa Stephen Masele akiteta jambo na Kiongozi wa chama cha Economic Freedom Fighters (EFF) cha Julius Malema Mei 11,2019