Mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Kampuni tanzu za IPP, Dk. Reginald Mengi, umewasili Kilimanjaro tayari kwa mazishi yatakayofanyika kesho Alhamisi Mei 9, kijijini kwake Nkuu Sinde, wilayani Hai mkoani Kilimanjaro.
Mwili wa Mengi uliwasili leo Jumatano Mei 8, saa 3:30 asubuhi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na kupokewa na viongozi mbalimbali akiwamo Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mughwira na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Jerry Muro.
Mughwira amesema Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, anatarajiwa kuongoza maelfu ya wakazi wa Mkoa wa Kilimanjaro na maeneo jirani.
Mbali na kiongozi huyo pia Spika wa Bunge, Job Ndugai, wabunge, mawaziri, wakuu wa mikoa, mabalozi pamoja na viongozi wa dini wanatarajiwa kushiriki katika mazishi hayo.
“Hadi sasa nimepata taarifa kwamba Rais atatuma Mwakilishi ambaye ni Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa atashiriki katika mazishi japo sijapata uthibitisho… pia Spika wa bunge letu atakuwepo pamoja na viongozi wengine mbalimbali wa kiserikali na dini,” amesema.
Social Plugin