Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAREKANI YAIKAMATA MELI YA KOREA KASKAZINI


Marekani imeikamata meli ya Korea Kaskazini ikiilaumu nchi hiyo kukiuka vikwazo vya kimataifa.

Idara ya haki ya Marekani imesema meli hiyo ilitumika kusafirisha makaa ya mawe ambayo ndiyo biashara kubwa ya taifa hilo licha ya kupigwa marufuku na Umoja wa Mataifa kuendelea kuyauza nje.

Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), meli hiyo ‘The Wise Honest’, ilikamatwa nchini Indonesia April mwaka jana, lakini Marekani ilitoa kibali cha kuikamata Julai mwaka huo.

Indonesia imeikabidhi Marekani meli hiyo na sasa inaelekea Marekani.

Hii ni mara ya kwanza Marekani kuikamata meli ya Korea Kaskazini kwa kukiuka vikwazo na hatua hiyo imekuja wakati ambapo uhusiano kati ya mataifa hayo mawili umedorora.

Mkutano kati ya kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un na Rais wa Marekani, Donald Trump uliisha bila makubaliano Februari mwaka huu, huku Marekani ikiisisitizia Korea Kaskazini kusitisha mpango wake wa nyuklia na nchi hiyo kwa upande wake ikitaka kuondolewa vikwazo vya kiuchumi kwanza.

Korea Kaskazini imetekeleza majaribio mawili ya makombora ya angani katika kipindi cha wiki moja katika kile kinachoonekana kuwa jaribio la kuishinikiza Marekani kufanya makubaliano.

Hata hivyo, maofisa wa Marekani wanasema uamuzi huo hautokani na majaribio ya makombora yaliyofanywa na Korea Kaskazini.

“Ofisi yetu iligundua mbinu ya Korea Kaskazini kuuza nje tani za makaa ya mawe ya kiwango cha juu kwa wanunuzi wa kigeni kwa kuficha asili ya meli The Wise Honest,” amesema mwendesha mashtaka wa Marekani, Goeffrey Berman.

"Mbinu hiyo iliifanya Korea Kaskazini kukwepa vikwazo mbali na kwamba meli hiyo ilitumika kuingiza mashine nzito nchini Korea Kaskazini ikisaidia uwezo wa taifa hilo na kuendeleza msururu wa ukiukaji wa vikwazo.”

Malipo ya utunzaji wa Wise Honest yanadaiwa kufanywa Marekani kupitia benki zisizojulikana, hivyo kuzipatia mamlaka za Marekani fursa ya kuchukua hatua hiyo.

Korea Kaskazini imekumbwa na msururu wa vikwazo vya Marekani na vile vya kimataifa kutokana na hatua yake ya kutengeneza silaha za nyuklia pamoja na kufanya majaribio ya silaha.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com