Marekani leo imeongeza kiwango cha ushuru kwa bidhaa za China hatua ambayo China imejibu mara moja ikisema italipiza kisasi. Mzozo huo umeshika kasi kabla ya siku ya pili ya mazungumzo ya kibiashara.
Rais Donald Trump alipata ufafanuzi kutoka kwa wajumbe wake wa kibiashara baada ya siku ya kwanza ya mazungumzo na upande wa China jana, lakini hakuchukua hatua yoyote kuhusu kutotangaza ushuru mpya – na hivyo kuua matumaini kuwa huenda kukawa na ahueni katika dakika za mwisho wakati mazungumzo hayo yakiendelea.
Dakika chache baada ya Marekani kuongeza kodi zake kali kwa bidhaa za China za thamani ya dola bilioni 200, kutoka asilimia 10 hadi 25, wizara ya biashara ya China ikasema "imesikitishwa sana” na uamuzi huo na kurudia ahadi yake ya kuchukua "hatua mwafaka za kulipiza kisasi”, bila kufafanua.
Kufuatia mgogoro wa zaidi ya mwaka mmoja, maafisa kutoka nchi hizo mbili kubwa kiuchumi duniani walirejea kwenye meza mazungumzo jana usiku, wakiongozwa na Naibu Waziri Mkuu wa China Liu He, Mwakilishi wa Biashara wa Marekani Robert Lighthizer na Waziri wa Fedha wa Marekani Steven Mnuchin.
Liu He alisema kuwa anataraji kuwa mazungumzo hayo yatakuwa ya wazi na ya tija kwa kila mmoja
"Bila shaka China inaamini kuwa kurudisha ushuru katika hali ya sasa sio suluhisho la tatizo hilo, bali kutaiumiza China, Marekani na ulimwengu mzima. Kwa hiyo kulitatua tatizo hilo ni kupitia njia imara ili mwishowe tupate suluhisho pekee la ushirikiano"
Licha ya matumaini kutoka kwa maafisa katika wiki za karibuni kuwa mazungumzo hayo yako kwenye mkondo wa kupata ufumbuzi, mivutano imezuka tena wiki hii baada ya Trump kwa hasira kuituhumu China kwa kujaribu kulegeza ahadi zake.
Shirika la Fedha la Kimataifa limetoa wito wa kupatikana ufumbuzi wa haraka, likionya kuwa mapambano hayo ya kibiashara ni "kitisho” kwa ukuaji wa uchumi duniani. Ushuru ulioongezwa utaathiri vifaa vya kielektroniki vya China, mashine, vipuri vya magari na samani.
Lakini kutokana na mchakato wa utekelezwaji wa viwango hivyo vya ushuru, bidhaa ambazo tayari zinapelekwa katika bandari za Marekani kabla ya usiku wa manane zitalipa tu kiwango cha awali cha asilimia 10 ya ushuru. Hayo ni kwa mujibu wa Ofisi ya Marekani ya Forodha na Ulinzi wa Mpakani.
Marekani inaishinikiza China kubadilisha sera zake kuhusu ulinzi wa hakimiliki za mali na kiwango kikubwa cha ruzuku kwa makampuni yanayomilikiwa na serikali, katika jaribio la kupunguza upungufu wa biashara.
Tangu mwaka jana, pande hizo mbili zimepandisha kodi za bidhaa za mwenzake za thamani ya zaidi ya dola bilioni 360 katika biashara ya pande mbili, na kuathiri bidhaa za kilimo za Marekani zinazouzwa China na kusababisha hasara kwa sekta za kutengeneza bidhaa za nchi zote mbili.
Taarifa ya wizara ya biashara ya China imesema wanatumai kuwa pande za Marekani na China zinaweza kukutana katikati na kufanya kazi pamoja kuyatatua matatizo yaliyopo kupitia ushirikiano na mazungumzo.
-DW
Social Plugin