Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAREKANI YAZIONYA NCHI ZA ULAYA KUHUSU MKAKATI WAO WA KUTOISHIRIKISHA MAREKANI KATIKA ULINZI

Moja ya hitilafu kuu baina ya Marekani na nchi za Ulaya wakati huu wa urais wa Donald Trump huko Marekani, ni misimamo ya kukinzana ya pande mbili kuhusu siasa na miundo ya ulinzi ya Ulaya na nafasi ya shirika la kijeshi la nchi za Magharibi, NATO.


Suala hilo limepelekea nchi za Ulaya kuangalia upya siasa zao za kiulinzi na kufikiria kuwa na ulinzi huru wa bara Ulaya usioihitajia Marekani. 

Hata hivyo serikali ya Trump haifurahishwi hata kidogo na jambo hilo. Kama kawaida yake, Trump anatumia lugha ya vitisho hata kwa waitifaki wakuu wa Marekani yaani nchi za Ulaya na kuzionya kuwa Washington itachukua hatua kali dhidi yao iwapo zitaamua kutekeleza mipango yao huru ya kiulinzi na kisilaha na kuiweka pembeni Marekani. 

Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon imetishia kuwa, iwapo Umoja wa Ulaya utaendelea kutekeleza kivyake-vyake mipango yake ya ulinzi, Washington itazichukulia hatua nchi hizo. 


Hii ina maana ya kwamba Marekani inaweza kutumia masuala ya kibiashara na kisiasa kukabiliana na nchi za Ulaya iwapo zitaendelea kuchukua misimamo ya kujitegemea katika mambo yao ya kiulinzi bila ya kuishirikisha nchi ya nje ya Umoja wa Ulaya kama Marekani.

Ellen Lord, naibu waziri wa ulinzi wa Marekani, mwanzoni mwa mwezi huu wa Mei 2019 alimuandikia barua Federica Mogherini, Mkuu wa Siasa za Kigeni na Kiusalama wa Umoja wa Ulaya na kulalamikia siasa huru za umoja huo za kujitegemea katika sekta ya ulinzi na silaha. 

Barua hiyo ilizitishia nchi za Ulaya kuwa Washington itazichukulia hatua iwapo zitaendelea na mipango yake ya kiulinzi isiyoishirikisha Marekani. 


Katika barua hiyo, Ellen Lord aliandika: Umoja wa Ulaya umetekeleza kivyake-vyake mipango yake ya kiulinzi na kisilaha, suala ambalo linatishia ushirikiano wa kijeshi wa Marekani na Ulaya na ni kinyume na makubaliano ya NATO.

Naibu huyo wa waziri wa ulinzi wa Marekani amesisitiza kuwa, kama Washington itajibu siasa hizo za Umoja wa Ulaya, basi majibu hayo hayatokuwa na mambo mazuri kwa washirika wa Washington huko Ulaya. 


Lord alidai kwenye barua yake hiyo kwamba: Sisi (Marekani) hatutaki tufike mahala tuchukue maamuzi kama hayo katika siku za usoni kwani uamuzi huo utakwenda sambamba na hasara ya mamilioni ya dola kwa mashirika ya kutengeneza silaha ya barani Ulaya.

Marekani imetoa vitisho hivyo katika hali ambayo tarehe 18 aprili 2019, Bunge la Ulaya lilipasisha mpango wa kuanzishwa mfuko maalumu wa kiulinzi wa Ulaya wenye thamani ya Euro bilioni 13 kwa ajili ya mwaka 2021 hadi 2027. Zaidi ya hayo, Washington inapinga masharti jumla yaliyoainishwa katika mpango wa ushirikiano wa kudumu unaojulikana kwa jina la PESCO. 

Kwa mujibu wa mpango huo, nchi 25 za Ulaya zimepanua miradi yao 34 ya silaha. Kinachoichukiza Marekani ni kwamba mpango huo wa PESCO unahusiana tu na Umoja wa Ulaya na kwamba nchi nyingine yoyote iliyoko nje ya eneo la umoja huo haiwezi kuwa na udhibiti wa silaha zinazozalishwa na kusafirishwa nje chini ya mpango huo. 

Miradi iliyoko chini ya mpango wa PESCO pia imeitia woga Marekani kwani mradi wowote ule lazima upate ridhaa ya nchi zote za Umoja wa Ulaya, sasa Washington ina hofu kwamba veto ya nchi moja tu ya Ulaya inaweza kukwamisha ushirikiano wake wa kijeshi na nchi yoyote ile ya Umoja wa Ulaya.


Juhudi za kuwa na kikosi huru cha kijeshi cha Ulaya, kuandaliwa mkakati wa kimataifa wa Umoja wa Ulaya na pia kuanzisha taasisi za kijeshi na kiusalama zinazohusiana na Ulaya tu ni kampeni ambayo imepata nguvu sana katika kipindi cha miaka minne iliyopita. 

Ujerumaini na Ufaransa ambazo ni miongoni mwa nchi muhimu zaidi za umoja wa Ulaya zina nafasi kubwa katika juhudi za kufanikisha jambo hilo na zinataka Umoja wa Ulaya uweze kujitegemea haraka sana kiulinzi. 

Lakini kama tulivyosema, Marekani haifurahishwi hata kidogo na jambo hilo. Katikati ya mwaka 2018, Donald Trump alimlaumu vikali Rais Nicolas Macron wa Ufaransa kwa kampeni yake ya kutaka bara la Ulaya liwe na jeshi lake huru la kujitegemea. 


Trump aliandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba: Macron amependekeza bara la Ulaya liwe na jeshi lake maalumu kwa ajili ya kujilinda mbele ya Marekani, China na Russia. Jambo hilo ni udhalilishaji mkubwa.

Hata hivyo inaonekana wazi kuwa Umoja wa Ulaya umekusudia kikweli-kweli kukabiliana na Marekani na NATO na kuhakikisha kuwa bara hilo linakuwa na uhuru wa kijeshi na kiulinzi haraka iwezekanavyo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com