MASAUNI AYATAKA MADHEHEBU YA DINI KOTE NCHINI KUENDELEA KUTII SHERIA ZA NCHI ILI KULINDA AMANI YA TANZANIA


Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
Naibu Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi Mhandisi  Hamad Masauni ametoa wito kwa viongozi   wa madhehebu ya dini  hapa nchini kuendelea kutiii sheria za nchi ili kuitunza amani ya Tanzania na kutojihusisha na Masuala ya Siasa. 


Mhandisi Masauni ametoa wito huo  Mei 4 ,2019  jijini Dodoma  wakati akifungua mkutano mkuu wa Dodoma Net Event unaoratibiwa na Kanisa la waadventista Wasabato na ukitarajiwa kuhitimishwa Mei 25 mwaka huu. 


Mhandisi Masauni amesema serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua mchango mkubwa unaofanywa na kanisa la waadventista Wasabato hivyo amelipongeza kwa kuwa na mchango mkubwa  kwa jamii katika kutoa masomo ya Afya,ujasiriamali,Kaya na Familia pamoja na kuwafundisha waumini wake kutii     Mamlaka za serikali hali ambayo inaendeleza kustawisha amani ya hapa nchini. 


Aidha Mhandisi Masauni ameyaasa madhehebu ya dini  Mengine hapa nchini kuiga mfano wa kanisa hilo kwa kuimarisha vijana   katika mazoezi na kuwafundisha uzalendo wa nchi yao      na akatoa mfano wa chama cha vijana watafuta njia wa kanisa hilo[Pathfinder]. 


Pia Mhandisi Masauni ametoa wito kwa madhehebu ya dini hapa nchini kushirikiana na serikali katika masuala ya kishirikina kwani yamekuwa yakisababisha kuawa watu wasiokuwa na hatia wakiwemo Watu wenye ualbino na vikongwe . 


Sanjari na hayo Mhandisi Masauni ametoa onyo kwa  baadhi ya vijana wanaotumia mitandao ya kijamii kukashfu na kutukana imani za watu wengine kwani inaweza kuhatarisha usalama wa Taifa huku akibainisha kuwa serikali itaendelea kuenzi na kuruhusu uhuru wa dini. 


Vilevile  Mhandisi Masauni amewaasa waumini wa kanisa la Waadventista Wasabato na watu wa Madhehebu mengine kuchangamkia Fursa zilizopo katika jiji la Dodoma kwa kuwekeza katika sekta za elimu,Afya  baada ya kurasmishwa kuwa Makao Makuu ya nchi. 


Akitoa neno  la shukrani ,mwenyekiti wa Union ya kaskazini mwa Tanzania kanisa la  Waadventista Wasabato ,Mch.Godwin Lekundayo ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kusisitiza uhuru wa Dini  kwani ndio msingi wa Amani huku akiiomba serikali kuingilia kati kwa baadhi ya taasisi hasa za shule kuwanyima uhuru wa kuabudu wanafunzi wake na kuwalazimisha kufanya mitihani siku za ibaada [Sabato]. 


Aidha Mch.Lekundayo ameishukuru serikali kwa kuendelea kupinga kuchanganya masuala ya siasa na  dini kwani yanaweza kuhatarisha amani ya nchi. 


Neno kuu la mkutano wa injili wa Dodoma Net Event ni Uzoefu wa Nguvu ya Mungu na mtoa neno ni .Mch.Baraka Muganda Mtanzania aishie nchini Marekani.
MWISHO.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post