Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

JINSI MASELE ALIVYOTIBUANA NA NDUGAI LEO BUNGENI...'AELEZA HUJUMA ZA KUTAKA ANG'OLEWE PAP'



Mbunge wa Shinyanga Mjini, Stephen Masele leo tarehe 23 Mei 2019, ametibuana na Job Ndugai, Spika wa Bunge.

Masele ambaye ni Makamu wa Rais wa Bunge la Afrika (PAP), ameshutumu mawasiliano ya Spika Ndugai na Roger Nkodo Dang, Rais wa Bunge la Afrika (PAP) kwamba, yalikuwa na malengo hasi kwake na nafasi yake ya umakamu wa rais wa PAP. 


Hata hivyo, Spika NdugaI amepinga kauli hiyo akieleza, kilichomfanya kumwita Masele nchini ni kuja kuhojiwa utovu wa nidhamu na si mgogoro wa PAP. 

Awali, Kamati ya Maadili ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge ilimtia hatia Masele kwa tuhuma zake za utovu wa nidhamu. Hata hivyo, Masele alipinga maelezo ya kamati hiyo.

Akizungumza bungeni Masele, ametoa hoja ya kukataa ripoti ya kamati hiyo iliyomtia hatiani, kuwekwa wazi ili Watanzania wajue nini alichoulizwa na kujibu.

Masele ametoa kauli hiyo alipopewa nafasi na Spika wa Bunge, Job Ndugai ya kuomba radhi Bunge, ndipo alipotumia muda huo kuliomba Bunge kuruhusu hansadi ya kikao cha mahojiano yake na kamati ya maadili.

“Kwa namna yoyote ile makosa yaliyorodhoshwa katika shitaka langu ningefurahi hansadi ya kikao ingeletwa kwenye Bunge hili ili wabunge na Watanzania wajue ukweli.

“Kwa mwenyekiti wa kamati hii, kuleta taarifa ambayo ina mapungufu, ninaomba nitoe hoja ya kukataa kamati hii na ripoti hii,” amesema Masele.

Licha ya kuikataa ripoti hiyo, Masele amesema sakata lake la kuitwa bungeni kwa ajili ya kuhojiwa ni mkakati wa Rais wa Bunge la Afrika (PAP), Roger Nkodo Dang wa kutaka kumng’oa madarakani kwa kumtumia Spika Ndugai ili kujinasua katika tuhuma za unyanyasaji wa ngono kwa watumishi wa Bunge hilo.

Mbele ya Bunge Masele amedai kuwa, ana uthibitisho kwamba Dang alifanya mawasiliano na Spika Ndugai kuhakikisha kwamba, yeye harudi PAP.

Amesema Dang alifanya mawasiliano hayo siku chache tangu alipoanza kusakamwa na tuhuma za unyanyasaji wanawake.

“Ninatambua Rais wa Afrika anafanya mawasiliano na wewe kuhakikisha mimi nisirudi kule PAP, mheshimiwa spika nasema haya kwa ujasiri sababu nina uhakika,” amesema Masele.

Katika hatua nyingine, Masele amesema, Dang alitumia madaraka yake vibaya kwa kuwasiliana na Spika Ndugai ilihali akijua kwamba, anafanyiwa uchunguzi.

“Barua aliyokuandikia inayokanusha haki zangu mimi kama mbunge na makamo wa rais wa PAP kwamba, ilifojiwa ni ile iliyoandikwa na rais ili kwenda kwa makamu wa pili wa rais, ilikwenda Algeria kuna makamu wa tatu wa rais,” amesema Masele na kuongeza:

“Kwenye ‘contect’ za barua ile inafanana, iweje ya kwangu iwe imefojiwa na zile hazijafojiwa rais yule aliandika barua ya kukanusha barua zake za mwanzo tarehe 11 Mei 2019, wakati yeye tulianza naye mgogoro tarehe 2 Mei, tumemuweka pembeni kwa uchunguzi lakini aliendelea kufanya makosa kuwasiliana na nyumbani wakati yuko katika uchunguzi.”

Masele ameomba radhi huku akisema kwamba, hana dhamira ya kumvunjia heshima Spika Ndugai kwa kutoitikia wito wake mara kadhaa, bali mazingira aliyokuwa nayo hayakumruhusu kuitikia wito wake.

“Kwa heshima nimekubali mimi ni kijana ninabeba dhamana nasimama kukuomba radhi, na ieleweke sikufanya mambo haya kwa makusudi kukuvunjia heshima sikufanya haya yanayoitwa makosa kwa nia yoyote ya kukudharau,” amesema Masele na kuongeza.

“Nilipokea mualiko wako saa 11 jioni saa za Afrika Kusini ikinitaka kesho yake nifike Dodoma, unatambua nilifika Afrika Kusini pasipokupewa nauli, ningepata wapi muda wa kulipa bili za hotelini na kukabidhi majukumu yangu na hususan Bunge lilikuwa na mogoro wa rais kutuhumiwa kwa kashfa ya ngono.”

Akijibu madai hayo ya Masele, Spika Ndugai amesema, Masele si mkweli kwa kuwa, kuhojiwa kwake hakutokani na mgogoro ulioko PAP.

“Si kweli hata kidogo, tuache vijitabia vya namna hiyo, nimalizie umeitwa nyumbani na unatokaje madaraka? waheshimiwa wabunge mimi ni spika wenu mtu mzima, niseme tabia za Masele za kusema uongo hata kwenye Bunge hili amesema uongo,” amesema Spika Ndugai.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com