Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amewataka Watanzania kutogombanishwa na kauli za viongozi hasa za kikabila na kidini huku akiwataka viongozi kutafakari maneno kabla ya kuyaongea kwani yanaweza kugawa watu na kuleta machafuko.
Aidha, Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai, amemuelezea aliyekuwa Mwenyekiti wa Kampuni Tanzu za IPP, Dk. Reginald Mengi alikuwa ni mtu asiyekata tamaa.
Mbowe ameyasema hayo Mei 9,2019 alipokuwa akitoa salamu za rambirambi katika ibada ya kumuaga aliyekuwa Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni tanzu za IPP, Dk. Reginald Mengi iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Moshi Mjini mkoani Kilimanjaro.
“Kuna kauli zinasemwa sana watu na kwa ukweli zinakera kwa vile mimi si mnafiki lazima niseme na nitasema hapa hapa mbele za watu.
“Tuna nchi moja ambayo tunastahili kupendana na kusaidiana, na kila mtu ana haki ya kumsaidia mwenzie, tusikubali kauli za viongozi zitugawe na hasa za kidini na kikabila, kauli ya kusema kuna makabila hayawezi kuwasaidia walemavu si nzuri na haikutupendeza kwa kweli, tujitafakari tunapotaka kuongea maneno,” amesema Mbowe.
Aidha Mbowe ametoa wito kwa kila aliyeguswa na msiba wa Dk. Mengi kuyaenzi yale yate aliyokuwa akiyatenda enzi za uhai wake kwani hiyo ndiyo njia pekee ya kumuenzi.
“Mzee Mengi ameshatangulia mbele za haki haitajalisha tuzungumze mema kiasi gani kumuhusu hatutamrejesha, ila tujitafakari na kuyaenzi yale aliyokuwa akiyafanya, alikuwa mnyeyekevu na kauli zake zilijenga, kupatanisha na kuleta matumaini lakini pia hakuwahi kukata tamaa,” amesema Mbowe.
Social Plugin