Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MDUDE CHADEMA ATAJA SABABU YA YEYE KUTEKWA NA WASIOJULIKANA


Mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mdude Nyagali amesema licha ya kupotea hivi karibuni kwa kile alichokidai kuwa ni kutokana na misimamo yake, alifikia hatua ya kukata tamaa ya kuishi.

Mdude ametoa kauli hiyo jijini Dar es salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari, ambapo ameeleza namna tukio hilo lilivyotokea.

"Mimi nilikata tamaa ya kuendelea kuishi na nilishaomba sala ili Mungu aipokee roho yangu, mwacheni Mungu aitwe Mungu, Mungu ni fundi", amesema Mdude.

Aidha Mdude amesema kuwa, "moja ya vitu ambavyo vinashangaza, sikuguswa maeneo mengine zaidi ya kupigwa kichwani lakini cha kushangaza zaidi, baada ya kupata fahamu nikakutwa nina majeraha mikononi na kwa mujibu wa wataalamu ni majeraha yalitokana na kufungwa pingu".

"Vitu vinavyothibitisha kuwa tukio langu la kutekwa ni la kisiasa, ni tweets zangu za mara ya mwisho kuhusu yule wakili aliyepotea", ameongeza Mdude.


Katika mkutano huo na wanahabari Mdude alimwaga machozi wakati akizungumzia namna alivyojikuta yupo porini baada ya waliomteka kumtupa.

“Nilijiuliza kosa langu ni lipi katika nchi hii na kama nina kosa mahakama si zipo kwa nini nifanyiwe hivi,” amesema Mdude huku akilia.

Mapema wiki mbili zilizopita zilienea taarifa juu ya kupotea kwa mwanachama huyo wa CHADEMA, lakini baadaye alipatikana wilayani Mbozi mkoani Mbeya akiwa hajitambui.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com