Serikali imesema haina mpango wa kuendelea kuvifungia vyombo vya habari vinavyokiuka kisheria kwenye utekelezaji wa majukumu na badala yake itaendelea kutumia njia ya majadiliano pale inapotokea changamoto ya kiutendaji.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbas aliyasema hayo jana jijini Dodoma wakati akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani 2019.
Dkt. Abbas alisema ni vyema wadau wa habari wakaunda kamati maalum itakayoketi na kujadiliana na Serikali kuhusiana na changamoto mbalimbali wanazodhani ni vikwazo kwenye utekelezaji wa majukumu yao ikiwemo vifungu na sheria za habari.
Aidha Dkt. Abbas aliwahimiza wadau wa habari kuzisoma na kuzielewa vyema sheria hususani Sheria ya Huduma za Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 ili wanapokutana na Serikali kwenye majadiliano wawe na uelewa wa kutosha kuelezea vifungu vyenye changamoto tofauti na hivi sasa ambapo baadhi wanalalamika bila kuweka wazi vifungu gani vina mapungufu.
Katika maadhimisho hayo, washiriki walipendekeza maazimio 16 ikiwemo kuunda kamati itakayoketi na Serikali kujadiliana baadhi ya changamoto zinazokwamisha uhuru wa habari kama vile kufungia vyombo vya habari pamoja na kanuni zenye vikwazo kwenye Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016.
Taasisi mbalimbali zilishiriki kufanikisha maadhimisho hayo ikiwemo MISA Tanzania, Ubalozi wa Marekani, Internews, FES, IMS, Umoja wa Mataifa, UTPC, TMF, TEF, UK Aid, TAMWA, MCT, Unesco na Serikali ya Tanzania huku kauli mbiu ikiwa ni “wajibu wa vyombo vya habari kwa demokrasia, tasnia ya habari na uchaguzi nyakati za upotoshaji wa taarifa”.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Dkt. Inmi Patterson akizungumza kwenye maadhimisho hayo ambapo alisisitiza juu ya uhuru wa vyombo vya habari katika kutimiza majukumu yake bila kuingiliwa.
Balozi wa Uingereza nchini Tanzania Mhe. Sarah Cooke akitoa salamu zake kwenye maadhmisho hayo.
Mkurugenzi wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Abubakary Karsan akichangia mada kwenye maadhimisho hayo.
Afisa Mawasiliano wa Umoja wa Mataifa ofisi ya Tanzania, Stella Vuzo akitoa salamu za Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres kwenye maadhimisho hayo.
Washiriki wa maadhimisho hayo wakifuatilia ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres kwa njia ya vidio.
Fuatilia matukio katika picha kwenye maadhimisho hayo.
Washiriki wa maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani 2019 kitaifa jijini Dodoma wamesimama kwa muda kama ishara ya kumuombea aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT) na pia mmiliki wa makampuni ya IPP, Dkt. Reginald Mengi aliyefariki usiku wa kuamkia jana nchini Dubai akiwa na miaka 77.
Washiriki wakiwa kwenye picha ya pamoja.
Washiriki wakifuatia mada kwenye maadhimisho hayo.
Mkurugenzi wa Misa Tanzania, Sengiyumva Gasirigwa (kulia) akisalimiana na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, Dkt. Hassan Abbas (kushoto) baada ya kuwasili kwenye maadhimisho hayo.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, Dkt. Hassan Abbas akiwa na Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Dkt. Inmi Patterson pamoja na viongozi kutoka taasisi mbalimbali kutembelea mabanda ya maonyesho ya kitaaluma kwenye maadhimisho hayo.
Wachezaji wa ngoma za asili kutoka kabila la Wagogo walinogesha mapokezi ya washiriki na viongozi mbalimbali.
Picha na KD Mula
Social Plugin