Tume ya Mawasiliano nchini Uganda imeagiza kufungwa kwa vituo 13 vya radio na televisheni pamoja na kufutwa kazi baadhi ya waandishi wa habari kwa ''kupotoshaji na kuchochea ghasia kwa kutangaza taarifa zenye ujumbe na hisia kali.
Hatua hiyo imechukuliwa saa chache baada ya mwanasiasa machachari wa upinzani na Mbunge wa Kyadondo Mashariki, Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine kukamatwa na kushtakiwa mahakamani.
Kuna madai kuwa huenda hatua hiyo imetokana na mtangazo ya moja kwa moja ya kukamatwa na kushtakiwa kwa Bobi Wine.
Kyagulanyi kwa sasa anazuiwa rumande na alitarajiwa kufikishwa tena mbele ya hakimu mkuu wa Mahakama ya Buganda Road leo Alhamisi.
Tume hiyo imesema vyombo hivyo vya habari vimekiuka kanuni ya kifungu cha 31 ibara ya 4 ya sheria ya mawasiliano ya Uganda ya mwaka 2013.
Hata hivyo, haikufafanua jinsi sheria hiyo ilivyokiukwa katika agizo lake kwa vyombo hivyo vya habari ambavyo ni vituo vya televisheni vya NBS, Bukedde TV, NTV, CBS FM na Capital FM.
Tume hiyo inataka hatua dhidi ya wazalishaji vipindi, wahariri wakuu na wasimamizi wa matangazo kusimamishwa kazi katika muda wa siku tatu.
"Hii ni kufuatia jinsi wanavyoshughulikia mada zinazorushwa hewani wakati wa matangazo ya moja kwa moja, habari za hivi punde na habari nyingine kwa ujumla bila kuzingatia kanuni," imesema UCC.
Ilivyopokelewa
Chama cha wanahabari nchini Uganda (UJA) kimeelezea kughadhabishwa na hatua hiyo.
''Wanahabari karibu 30 wanakabiliwa na tishio la kufutwa kazi na hili litakuwa na athari hasi si kwa taaluma zao tu, bali mamilioni ya Waganda watakosa huduma ya kupashwa habari,'' imesema taarifa ya chama hicho.
UJA imesema Serikali kupitia mashirika yake ya udhibiti wa mawasiliano inatakiwa kuheshimu uhuru wa vyombo vya habari.
Baadhi ya watu pia wameileza BBC kuwa hatua hiyo inaleta taswira mbaya kwa Uganda wakati ulimwengu unapoadhimisha siku ya kimataifa ya uhuru wa vyombo vya habari duniani.
Tume hiyo imedai kuwa iliwahi kutoa onyo kuhusiana na suala hilo lakini baadhi ya vyombo vya habari havikutilia maanani onyo hilo.
Mamlaka nchini Uganda imekuwa ikijaribu kuzima umaarufu wa mwanamuziki na mbunge huyo kwa kuvilazimisha vyombo vya habari kutomtangaza.
Umaarufu wa Bobi Wine umemfanya kuonekana tishio kwa utawala wa Rais Yoweri Museveni ambaye huenda akagombea tena urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2021 ikiwa ni miaka 35 tangu aingie madarakani.