Quito, Ecuador, AFP. Raia wa Japan amehukumiwa kifungo cha miaka miwili jela nchini Ecuador baada ya kupatikana na hatia ya kujaribu kusafirisha nje rundo la wadudu wa aina tofauti, kama buibui na mende, maofisa wa serikali wamesema.
Mtu huyo alikamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Quito mwezi Machi akiwa na wadudu 248, ambao ni mende, dondora, nyuki na vipepeo aliowaweka kwenye sanduku, msemaji wa wizara ya mazingira alisema.
Mtu huyo ambaye alijulikana kwa jina moja la Hirokazu S, pia ametozwa faini ya dola 4,000 na kuamriwa aombe radhi hadharani kwa kutumia gazeti la kitaifa, ilisema wizara hiyo.
Ecuador, nchi ndogo ya Amerika Kusini yenye watu milioni 17, ni moja ya nchi zenye aina nyingi za viumbe.
mamlaka zimepiga marufuku kukamata na kuuza wanyama mwitu, lakini biashara haramu inaendelea katika maeneo yote nchini humo.
Mjapani huyo alikuwa analenga kuwapeleka wadudu hao Hokkaido, kaskazini mwa Japan.
Social Plugin