Hatimaye mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP Limited, Dkt. Reginald Mengi umezikwa katika makaburi ya familia yao yaliyopo nyumbani kwa wazazi wake, Nkuu, Machame, wilayani Hai mkoani Kilimanjaro, leo Alhamisi, Mei 9, 2019.
Mazishi ya Dkt. Mengi ambayo yameanza na ibada katika Kanisa la KKKT, Usharika wa Moshi Mjini, yamehudhuriwa na mamia ya waombolezaji wakiongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Spika Job Ndugai, mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya, wabunge, viongozi wa dini, siasa na taasisi mbalimbali za Serikali na binafsi.
Mengi ameacha simanzi kubwa kwa Watanzania wengi kutokana na ukarimu wake katika kuwasaidia watu mbalimbali wakiwemo wenye ulemavu, vijana, wazee na maskini ili kujikwamua katika wimbi la umaskini.
Akihubiri wakati wa ibada ya kuaga mwili huo, Askofu Mkuu wa KKKT, Dkt. Fredrick Shoo amemtaka Spika Job Ndugai, Bunge na wote wenye mamlaka wakatende haki kwa watu wote.
“Nashukuru Mheshimiwa Ndugai uko hapa. Kazi ya Bunge ni kutetea maslahi ya wananchi. Teteeni maslahi ya wananchi mnaowawakilisha, kama kweli tunasema tumejifunza kutoka kwa Dk Mengi,” amesema Dkt. Shoo.
Mengi alifariki dunia usiku wa kuamkia Alhamisi iliyopita, Mei 2, 2019, nchini Dubai katika Falme za Kiarabu na mwili wake uliwasili nchini Jumatatu, Mei 6 kabla kuagwa Karimjee na kusafirishwa kwenda Machame ambako umezikwa leo.
Ameacha mjane, Jacqueline Ntuyabilwe, watoto wanne ambapo watatu ni wa kiume na mmoja wa kike.