Na Bakari Chijumba.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Timu ya SimbaSC , Mo Dewji amesema baada ya Kocha Mkuu wa Klabu hiyo,Patrick Aussems kutimiza malengo yaliyowekwa na Klabu,tayari bodi imepanga kukaa naye na kumuongezea mkataba mpya ili aendelee kuifundisha Simba SC.
Kuhusu ahadi ya Milioni 5 kwa kila mchezaji baada ya ubingwa, Mo Dewji amesema hakutoa ahadi hiyo bali alisema atatoa zawadi ya Pikipiki(Boxer) kwa kila mchezaji na tayari amewapa ili kuinua vipato vyao,MO amesema wakiweka watu wa kuziendesha zitawaingizia kipato.
Dewji amesema ameshaongea na viongozi wa klabu ya DC United ya Marekani na kuwaomba wakafanye maandalizi ya msimu ujao huko pia wacheze nao na timu nyingine za LMS au kwenda nchini Ureno ili wakacheze na timu za huko.
Katika hatua nyingine MO ameipongeza Klabu ya Yanga kwa kuongeza ushindani kwenye Ligi.
"Naipongeza Yanga SC kwa kuleta ushindani mkubwa kwenye Ligi yetu na nichukue fursa hii kuwapongeza viongozi wapya wa Yanga SC na niwaombee wajipange ili waweze kufanikiwa, najua msimu ujao utakuwa mgumu sana"amesema Mo na kuongeza;
''Kwenye usajili tupo makini sana,leo tunapata ripoti ya kocha juu ya wachezaji wa nyumbani anaowataka,pia katika wachezaji 10 wa kigeni mpaka leo usiku kocha atatuambia anabaki na nani na nani waondoke..Simba itakuwa kwenye soko la kushindana na timu kama Mazembe na Al Ahly"
''Katika kusajili, kuna wachezaji wengine tutawatoa kwa mkopo lengo ni kutengeneza timu yenye ushindani zaidi na tutajitahidi usajili wetu uende sawa na vilabu vikubwa Afrika ili tukafanye vizuri kwenye Ligi ya Mabingwa''
Social Plugin