Mwanafunzi aliyeunguzwa maji ya moto
Binti mwenye umri wa miaka 16,mwanafunzi wa darasa la saba shule ya msingi Kashenge iliyoko katika Manispaa ya Bukoba amelazwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Kagera akiuguza majeraha anayodai kuyapata baada ya kuunguzwa kwa maji ya moto na mama yake wa kambo.
Akizungumza kwa shida katika wodi namba kumi iliyoko katika hospitali hiyo, binti huyo alisema kuwa mama huyo wa kambo alifika nyumbani na kumkuta amepika viazi akamuuliza kwa nini alipika viazi bila kuambiwa, ndipo akammwagia maji ya moto.
“Baada ya kuingia jikoni akakuta nimepika viazi akachukua sufuria na kunimwagia maji ya moto, niliamua kuondoka na kuingia ndani, akaja mdogo wangu akaniambia twende kwa Afisa Mtendaji lakini hatukumkuta” alisema.
Binti huyo alieleza kuwa mama yao mzazi alitengana na baba yao na kuwaacha wakiwa watano yeye na wadogo zake wanne.
Afisa muuguzi msaidizi wa wodi namba kumi upande wa upasuaji Edith Ezekiel alisema walimpokea binti huyo Mei 22,2019 akiwa ameunguzwa mkono wa kulia, titi na sehemu za bega, na kuwa hali yake kwa sasa sio mbaya amesafishwa kidonda na anaendelea na matibabu.
“Nilimsafisha kidonda naona kinaendelea vizuri, mkono umejikunja lakini nimejaribu kuunyoosha, sasa unaweza kunyooka na kujikunja”, alisema Ezekiel.
Mama mzazi binti huyo aliyefahamika kwa jina la Alodia au mama Judith alisema akiwa nyumbani kwake wilayani Muleba alipata taarifa kwa njia ya simu kutoka kwa jirani na wanakoishi watoto hao, na kumwambia mtoto wake ameunguzwa kwa maji ya moto.
“Nilipopata taarifa hizo nikafika kwa ajili ya kumuona nikakuta kweli ameunguzwa na sasa yuko hospitali anaendelea na matibabu, tukisubiri hatua nyingine za kisheria” alisema.
Akizungumzia tukio hilo ambalo limeripotiwa polisi na kufunguliwa jalada la kujeruhi namba RB/2466/19, kamanda wa polisi mkoani Kagera Revocatus Malimi amesema kuwa atatoa taarifa rasmi Mei 24 mwaka huu.
Social Plugin