MSEMAJI WA SERIKALI: MAONO NA MTAZAMO WA RAIS MAGUFULI YAZIDI KUPAISHA MAKUSANYO YA MAPATO YA MADINI


Na Mwandishi Wetu,MAELEZO
SERIKALI imesema maono na mtazamo yakinifu wa Rais Dkt. John Magufuli katika usimamizi na ufuatiliaji wa sekta ya madini, umewezesha ongezeko maradufu la makusanyo ya mapato ya sekta hiyo kutoka Tsh Bilioni 210 mwaka 2015/16 hadi kufikia Tsh Bilioni 302 kwa mwaka 2018/19 na kuifanya Tanzania kuzidi kujijenga Kiuchumi.


Akizungumza na waandishi wa vyombo vya habari leo Alhamisi (Mei 30, 2019) Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi, alisema Serikali ya Awamu ya Tano inafanya kazi kisayansi na itahakikisha rasilimali za nchi zinaendelea kulindwa ili ziweze kuleta manufaa kwa Watanzania wote.

Dkt. Abbasi alisema mara baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kuingia madarakani Novemba 2015, ilifanya mageuzi mbalmbali katika usimamizi na ufuatiliaji wa rasilimali za madini, kwani huko nyuma Serikali ilikuwa ikipoteza kiasi kikubwa cha fedha na kuamua kuchukua hatua stahiki ikiwemo kufanya mabadiliko katika Sheria ya Madini ya mwaka 2010.

“Tulipofanya marekebisho katika sheria yetu ya madini mwaka 2017, matokeo tumeanza kuyaona kwani tumedhibiti mianya yote ya upotevu wa mapato yetu na kuanza kusimamia kwa umakini mkubwa utoroshaji mkubwa wa madini ambapo ilisababisha Serikali kupoteza kiasi kikubwa cha mapato” alisema Dkt. Abbasi.

Akitolea mfano Dkt. Abbasi alisema kufuatia agizo la Rais Dkt. John Magufuli la kuanzishwa kwa masoko ya madini ambayo ni utekelezaji wa sheria ya madini ya mwaka 2017, hadi sasa kuna jumla ya masoko 24 ambayo yamekuwa yakithibiti ubora, thamani na takwimu za madini nchini, ambapo soko la kwanza lilianzishwa Mkoani Geita, mwezi Machi mwaka huu.

Aidha Dkt. Abbasi alisema Takwimu za jumla za uzalishaji wa dhahabu katika kipindi cha miezi miwili , mkoani Geita kuanzia mwezi Machi hadi Mei, mwaka huu zinaonyesha kuwa uzalishaji umeongezeka kwa kiasi kikubwa na kufikia kilo 312.65 za dhahabu ukilinganisha na uzalishaji wa dhahabu  kilo 259.12 zilizokuwa zikizalishwa kabla ya masoko hayo.

“Mwezi April, pekee uliweka rekodi ya Geita kwa kuzalisha kilo 200 ambazo hazijapata kufikiwa mkoani humo kwa wachimbaji wadogo na wa kati na kwa Takwimu za Mei mwezi mwaka huu zinazidi kuthibitisha kuwa Watanzania wanapaswa kuendelea kumuombea na kumuunga mkono Rais Magufuli” alisema Dkt Abbasi.

Kwa mujibu wa Dkt. Abbasi alisema eneo lingine la mageuzi yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika sekta ya madini ni pamoja na maamuzi iliyochukua ya kujenga ukuta kuzunguka eneo la wachimbaji wa Madini ya Tanzanite Mkoani Manyara ambao Serikali iliweka mifumo ya masoko na ukaguzi, na hivyo kuchangia ongezeko la mapato ya wachimbaji wadogo na Serikali kwa ujumla.

Akifafanua zaidi Dkt. Abbasi alisema uzalishaji wa madini ya Tanzanite kutoka kwa wachimbaji wadogo ulioripotiwa kwa mwaka 2016 ulikuwa kilo 164.6 na kilo 147 kwa mwaka 2017, ambapo Serikali iliweka kukusanya kiasi cha Tsh Milioni 71 (2016) na Tsh Milioni 166 (2017), lakini uzalishaji huo uliongezeka maradufu mara baada ya Serikali kujenga ukuta huo.

“Uzalishaji uliongeza sana mara baada ya ujenzi wa ukuta kwani Kilo 781.2 zilizalishwa mwaka 2018 na kuiingizia Serikali mapato ya Tsh Bilioni 1.43 na uzalishaji kwa mwaka 2019 katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Mei ulikuwa kilo 1086.05 zenye thamani ya Tsh Bilioni 1.422” alisema Dkt. Abbasi.

Aliongeza kuwa mabadiliko hayo yameanza kuleta faida kwa nchi ambapo kwa sasa nchi nyingi za Afrika zimeanza kuiga mageuzi yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano ikiwemo kupitia upya mikataba na wawekezaji na pia watafiti mbalimbali wanairejea Tanzania inayogeuza “laana” ya madini kuwa “Baraka” ya Madini.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post