Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma
Mwenyekiti wa Bunge La Jamhuri ya Muungano Wa Tanzania Mhe.Nagma Giga ameishauri serikali ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Tanzania bara kukaa pamoja kuona namna ya kuwa na Mtaala mmoja wa Elimu ili kuinua na kuboresha kiwango cha ufaulu kwa pande zote mbili.
Mhe.Giga amesema hayo leo Mei 22,2019 Bungeni jijini Dodoma wakati akielekeza swali la nyongeza kwa wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ambapo amesema pamekuwepo na mkanganyiko mkubwa katika suala la Elimu kwa Zanzibar na Tanzania Bara kutokana na Mitaala ya Elimu kutofautiana hali ambayo husababisha Zanzibar kuwa nyuma.
Akijibu Swali hilo Naibu Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia ,Mhe.Wiliam Ole Nasha amesema serikali itaangalia namna ya kufanya ili kuweza kutoa mitaala ya elimu inayofanana ili kuondoa mkanganyiko kwa pande zote mbili za Muungano kati ya Tanzania bara na Zanzibar.
Aidha.Mhe.Wiliam Ole Nasha amesema serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuongeza ufaulu katika ngazi mbalimbali za elimu ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa miundo mbinu ambapo kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2018/209 zaidi ya Tsh. Bilioni 93.8 zimetumika kuboreha miundombinu ya shule 588.
Pia amesema serikali imeendelea kuimarisha Idara ya Uthibiti Ubora wa shule ambapo imenunua na kusambaza magari 45 ya uthibiti Ubora wa shule na pikipiki 2,897 kwa ajili ya Maafisa Elimu Kata kwa mwaka 2019/2020 huku ikitarajia kujenga ofisi 100 za wathibiti Ubora wa Shule na kuongeza idadi ya watumishi.
Ikumbukwe kuwa ufaulu wa wanafunzi katika kidato cha nne umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka ambapo mwaka 2018 asilimia 78.36% ya watahiniwa walifaulu ikilinganishwa na 77.09 % ya mwaka 2017 ,70.35 %ya mwaka 2016 na 67.91 % ya mwaka 2015.
Social Plugin