Aliyekuwa mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu amesimulia namna alivyokamatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na kuhojiwa kwa saa kadhaa kabla ya kuachiwa kwa dhamana leo mchana Mei 28, 2019 na kutakiwa kuripoti polisi kesho.
Nyalandu amesema alikamatwa jana saa 8 mchana akiwa kwenye kikao cha ndani na vijana 29 katika kijiji cha Itaja jimbo la Singida Kaskazini.
Amesema walivamiwa na watu walioanza kuuliza alipo Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Singida, Shaban Lyimo ambaye alisimama na kuwaeleza watu hao kuwa walikuwa katika kikao cha ndani cha Chadema.
“Kwanza walituliza kibali (cha kikao), Lyimo akawajibu kuwa hatuna na ni kikao cha ndani hakihitaji kibali. Wakasema kuwa wao wametoka Takukuru Mkoa wanawahitaji watu wakaninyooshea kidole mimi (Nyalandu) na David Jumbe pamoja na mwenyekiti (Lyimo),” amesema Nyalandu.
Amesema walielezwa kuwa wanahitajika kwa ajili ya mahojiano Singida mjini na walipofika wakaelezwa kuwa wanafuatilia masuala ya rushwa.
“Tulipofika polisi tulihojiwa zaidi ya masaa mawili tukapewa dhamana ilikuwa imefika saa 4 usiku tuliambiwa kwamba twende kisha turudi asubuhi (leo), wakati tukijiandaa kuondoka, mkuu wa kile kituo akapigiwa simu na kutakiwa kufuta dhamana zetu, hivyo tukalala ndani hadi leo.”
“Kwa tunachofanyiwa ni dhahiri watu wanakihofia Chadema ndio maana wanatumika kutubughudhi na kutukatisha tamaa, kwa kuwa wakati tunafanya kikao pale pembeni mwa barabara kulikuwa na wanachama wa chama fulani (akakitaja) wakiwa katika kikao kama chetu lakini huko hawakwenda,” amesema Nyalandu.
Na Gasper Andrew, Mwananchi