Maafisa wa wanyama pori wamesambaza picha za nyoka mwenye macho matatu aliyepatikana katikati ya barabara kaskazini mwa Australia.
Shirika la huduma kwa wanyama pori na bustani za wanyama Northern Territory Parks and Wildlife Service wameeleza kwamba nyoka huyo ambaye picha zake zilisambaa pakubwa katika mitandao ya kijamii, ni wa "kustaajabisha".
Amepewa jina la Monty Python, nyoka huyo aina ya chatu alifariki wiki kadhaa tu baada ya kugunduliwa mnamo Machi,2019.
Wataalamu wanasema jicho la tatu la nyoka huyo lililo juu ya kichwa chake limeonekana kuwa ni mabadiliko ya asili
Maafisa walimgundua nyoka huyo katika mji wa Humpty Doo, 40km kusini mashariki mwa Darwin.
Ana urefu wa 15 inchi na alikuwa akipata tabu kula chakula kutokana na ulemavu wake, maafisa wameiambia BBC.
'Hali' ya kawaida
Shirika hilo la huduma kwa wanyama pori limesema picha za X-ray zimeonyesha kwamba hakuwa na vichwa viwili kwa pamoja.
"Badala yake alionekana kuwa na fuvu moja la kichwa na jicho la ziada ukijumlisha, macho matatu yanayofanya kazi sawasawa," lilieleza kwenye Facebook.Alikuwa akipata tabu kula chakula kutokana na ulemavu wake
Mtaalamu wa nyoka Profesa Bryan Fry amesema mabadiliko ya maumbile ni sehemu ya kawaida ya kuumbwa.
"Kila mtoto hupitia mabadiliko ya kiwango fulani - huyu alishuhudia mabadiliko yasio ya kawaida," amesema Profesa Fry, kutoka chuo kikuu cha Queensland.
"Sijaona nyoka mwenye macho matatu awali, lakini tumeona chatu mwenye vichwa viwili katika maabara yetu - ni aina tofuati ya mabadiliko kama tunavyoona kwa pacha wachanga wanaozaliwa wakishikana."
Ameashiria kwamba huenda jicho hilo la tatu likawa " sehemu ya mwisho ya pacha wa nyoka huyo aliyefyonzwa".
Chanzo - BBC
Social Plugin