Washambuliaji nyota wa Simba, Emmanuel Okwi na Messy Kagere wameweka rekodi ya kufunga mabao sita yaani hat trick mbili ndani ya mechi moja.
Wachezaji hao wote wenye asili ya Uganda kwa kuwa Okwi ni Mganda na Kagere ni Mnyarwanda mwenye asili ya Uganda, wamefunga bao hizo sita wakati Simba ikiitwanga Coastal Union kwa mabao 8-1 katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyomalizika hivi punde kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Mabao hayo, yanamfanya Kagere kufikisha mabao 20 msimu katika ligi kuu akifikia rekodi ya mabao 20 ya Okwi msimu uliopita lakini akibakiza bao moja kufikia idadi ya mabao 21 aliyofunga Amissi Tambwe msimu wa 2015/16 akiwa mfungaji bora.
Kwa mabao hayo 14, Okwi naye amemfikia nahodha wake John Bocco aliyekuwa benchi katika mechi ya leo akishuhudia 'vijana wake" wakiwagaragaza Wagosi wa Kaya.
Mabao mengine yalifungwa na Hassan Dilunga na Cleotus Chama raia wa Zambia na kuifanya Simba iandike ushindi huo mnono zaidi.
Kwa ushindi wa leo, Simba imefikisha pointi 81 na kupaa kileleni ikiwaacha Yanga wenye pointi 80 waliokuwa wamekaa kileleni kwa muda mrefu zaidi.
Yanga wamecheza 34 huku Simba wakiwa wamefikisha mechi 31 baada ya kucheza mechi yao ambayo wametoa kipigo kikali kwa Wagosi wa Kaya.
Social Plugin