Mwendesha mashtaka wa umma nchini Sudan amemshitaki rais aliyeondolewa madarakani Omar al-Bashir kwa makosa ya kuchochea na kuhusika na mauaji ya waandamanaji.
Mashtaka hayo yametokana na uchunguzi uliofanywa kuhusu kifo cha ddaktari aliyeuawa wakati wa maandamano yaliyosababisha kumalizika kwa utawala wake mwezi uliopita.
Hatma ya Bwana Bashir haijawa wazi. Aliripotiwa kutiwa nguvuni mara baada ya kupinduliwa.
Anakabiliwa pia na uchunguzi juu ya madai ya wizi wa pesa na kudhamini ugaidi
Mnamo mwezi Disemba, waandamanaji walianza maandamanano dhidi ya uamuzi wa serikali wa kupandisha mara tatu kwa bei ya mkate.
Maandamano hayo ghafla yalibadilika kuwa hasira iliyosambaa kote nchini dhidi ya kiongozi huyo ambaye alikuwa mamlakani kwa miaka 30, yakiongozwa na madaktari.
Maandamano yalifanyika kwa wiki tano na shahidi mmoja anasema tarehe 17 Januari, vikosi vya usalama viliwafyatulia risasi waandamanaji na kumuua daktari.
Baadaye waandamanaji waliamua kufanya maandamano yao kwa kuketi nje ya makao makuu ya kijeshi, na kudai jeshi limg'oe mamlakani rais.
Baraza la kijeshi lilichukua mamlaka ya nchi tarehe 11 Aprili, lakini waandamanaji wanasisitiza kwamba jeshi lazima likabidhi utawala wa nchi kwa raia.
Social Plugin